Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Sadio Mane ameanza kuipigia hesabu ofa ya klabu ya Al-Nasr ya Saudi Arabia ambayo imeonesha nia ya kumsajili.
Mane alijiunga na Bayern kabla ya msimu uliopita wa 2022-23 kwa ada ya Pauni 35 milioni akitokea Liverpool lakini hakuweza kuonesha makali aliyokuwa nayo wakati akiwa Liverpool na zipo habari kwamba Bayern ipo tayari kumpiga bei.
Kocha wa timu hiyo, Thomas Tuchel anaonekana kupoteza matumaini na mchezaji huyo na hivyo yupo tayari kufanya biashara na klabu yoyote itakayojitokeza wakati Mane naye inadaiwa tayari amefanya mazungumzo ya awali na mabosi wa Al-Nasr.
Akiwa Liverpool, Mane alijipatia mafanikio kwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England kabla ya kutimkia Bayern akidai kwamba ulikuwa wakati sahihi kwake kupata changamoto mpya ingawa mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa.
Kibaya zaidi, Mane aliingia katika mzozo na mchezaji mwenzake wa Bayern, Leroy Sane akidaiwa kumpiga ngumi Aprili mwaka huu baada ya timu hiyo kushindwa kutamba katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Man City.
Tukio hilo lilimfanya aondolewe kwenye kikosi cha Bayern na kutozwa faini ingawa baadaye alirudishwa lakini hadi mwisho wa msimu aliishia kufunga mabao 12 katika mechi 38.
Kocha Tuchel aliwahi kusema kwamba mambo hayajawa rahisi kwa Mane kwenye kikosi cha kwanza na ushindani umekuwa mkubwa mno kwake na mchezaji huyo anafahamu hilo na anaujua msimamo wa klabu.
Ikitokea mpango wa Mane kwenda klabu ya Al-Nasr ukafanikiwa, mchezaji huyo atakuwa ameungana na winga wa zamani wa klabu za Real Madrid na Mancheter United, Cristiano Ronaldo.
Kimataifa Saudi Arabia kwamvutia Mane
Saudi Arabia kwamvutia Mane
Read also