Na Hassan Kingu
Michezo ya Ngao ya Jamii inayoashiria kufunguliwa pazia la msimu mpya wa soka wa 2023-24 inayotarajia kupigwa Agosti, mwaka huu inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.
Miongoni mwa yanayofanya mechi hizo zisubiriwe kwa hamu mno safari hii ni mabadiliko au ongezeko la ushiriki wa timu katika mechi ya Ngao kutoka mbili mpaka kufikia nne.
Mechi hazitachezwa kwa mtindo wa bingwa wa Ligi Kuu NBC dhidi ya bingwa wa Kombe la FA (ASFC), bali itachezwa na timu zilizomaliza kwenye nafasi nne za juu kwenye ligi ya msimu uliopita.
Bingwa wa ligi, Yanga itaumana na Azam FC iliyomaliza nafasi ya tatu, Agosti 9 kisha Simba iliyomaliza ya pili itacheza na Singida Fountain Gate Agosti 10, kabla ya mchezo wa fainali utakaochezwa Agosti 13. Mechi zote hizo zikipigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Msisimko ni mkubwa kuelekea maandalizi ya mechi hizo, kwa kutambua ugumu na ushindani wa kila timu tayari timu hizi zimeanza kambi ya msimu ujao lakini mtihani wao wa kwanza ukiwa ni kufanya vizuri kwenye Ngao kwanza.
Taswira Kimataifa
Mashabiki wanatarajia ushindani mkubwa baina ya timu hizi kwa kuwa zote msimu ujao zitawakilisha taifa kwenye michuano miwili mikubwa ya klabu Afrika. Yanga na Simba zitashiriki Ligi ya Mabingwa, Azam na Singida zitapambana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya msimu kuanza, mashabiki watashuhudia ladha ya timu zinazoshiriki michuano hiyo zikiumana zenyewe kwa zenyewe na kupeana changamoto ya uhakika na kufahamu ugumu wa huko waendako mapema.
Joto ya Jiwe Mapema
Timu za Yanga na Azam zitaingia kwenye kinyang’anyiro cha Ngao hiyo zikiwa na makocha wakuu wapya. Msenegali, Youssouph Dabo wa Azam na Muargentina, Migeul Gamondi wataziongoza timu zao kwa mara ya kwanza kwenye mashindano maalumu.
Yawezekana wamekuwa wakisikia ‘joto ya jiwe’ ya mechi za timu hizi kubwa zinapokutana lakini sasa wanakwenda kuishi katika presha hiyo kwa mara ya kwanza huku wakihitaji matokeo bora kwa ajili ya kuanza vyema msimu.

Kulingana na ubora wa vikosi vya timu shiriki, ni wazi tutashuhudia mbinu na silaha nzito za makocha hawa mapema kabla ya ligi kuanza ili kuonesha umwamba wao mbele ya wababe wengine wa ligi au vinginevyo tushuhudie mapungufu yao mapema kwenye mechi nzito.
Kocha wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameanza kuwa mzoefu na mechi hizi kali za Tanzania kutokana na uwepo wake tangu katikati ya msimu uliopita lakini hili ni jaribio jingine kwake kuelekea msimu ujao.
Kocha wa Singida, Hans Pluijm raia wa Uholanzi ndiye mkongwe katika haya mapambano. Miaka ya nyuma kwa nyakati tofauti aliwahi kuzinoa Yanga na Azam na kuonesha ‘umafia’ wake.
Ingawa hivi karibuni kwa mujibu wa matokeo anaonekana kupungukiwa mbinu katika mechi ngumu kama hizi, lakini ukongwe wake unaweza kuwa kikwazo pia kwa Robertinho, Gamondi au Dabo.
Wachezaji wapya
Kingine ni kuonekana kwa wachezaji wapya zaidi ya mara moja kabla ya ligi kuanza. Imezoeleka wachezaji wapya wa hizi timu kuelekea msimu ujao huonekana kiushindani kabla ya kuanza kwa ligi kwenye mechi moja ya Ngao lakini wataonekana zaidi ya mara moja.
Dakika 180 kwa maana ya mechi mbili ni ujazo tosha wa kumtazama na kumfanyia tathmini ya kina mchezaji mpya hasa kwenye mechi za ushindani kama hizo.
Mashabiki wa Simba watawashuhudia nyota wao wapya waliotikisa kusajiliwa hivi karibuni kama beki Mcameroon, Che Fondoh Malone, washambuliaji Mnyarwanda, Willy Onana na Muivorycoast, Aubin Kramo ambao wametikisa vilivyo ligi walizotoka.

Yanga pia ukiachana na usajili wa Nickson Kibabage au Jonas Mkude wanaofahamika kama ilivyo kwa David Kameta ‘Duchu’ aliyerejea Simba lakini pia mashabiki wao wana hamu ya kumuona aliyekuwa nahodha wa SC Villa, beki Gift Fred ‘Giggy’ aoneshe makucha yake.
Vilevile, Azam iliyoko Sousse, Tunisia ilikoweka kambi pia itahitaji kuonesha kama kweli imelamba ‘dume’ katika usajili wa kiungo mshambuliaji wa Gambia, Djibril Sillah, beki Cheikh Sidibe na Allasane Diao ambao wote ni raia wa Senegal. Usisahau Feisal Salum ‘Fei Toto’ pia ni usajili mpya wa Azam.
Na Singida imeshamnasa beki Mkenya, Joash Onyango aliyekuwa Simba, Yahya Mbegu aliyekuwa Ihefu na inatajwa kumalizana na kipa Beno Kakolanya aliyekuwa Simba.
Kimsingi Singida bado haijaonesha makucha upande wa sura ‘mpya’ kwenye kikosi chao lakini bado dirisha liko wazi na pengine lolote linaweza kutokea kabla ya siku ya michezo yenyewe.
Fursa kwa timu nyingine
Wakati timu hizi zinaminyana uwanjani, zilizobaki ambazo zilimaliza nafasi ya tano kwenda chini na zile zilizopanda daraja ambazo hazishiriki mechi hizi zina nafasi ya kuwaona mapema wababe hawa na kupata picha ya watakachokwenda kukutana nacho baada ya msimu kuanza.
Ni fursa kwao kurekebisha baadhi ya sehemu vikosini mwao baada ya kushuhudia mechi za timu hizi nne.
Timu zote 16 zinafanana ngazi ya ushindani kwa maana ya ushiriki wa ligi moja lakini hizi nne za juu ni dhahiri zina vingi vya ziada hata kwa kuzipa heshima tu ya ushiriki wao kimataifa msimu ujao, hivyo ni kitu kizuri kuwatazama na kudadavua machache kutoka kwao.
Hamasa mpya
Ushiriki wa timu nne pia ni kama hamasa mpya kwa soka la Tanzania kwa kuwa sasa mbali na timu zinazomaliza kwenye nne bora kushiriki michuano ya Caf (Shirikisho la Soka Afrika) lakini pia zitakata tiketi ya kucheza Ngao ya Jamii.
Jambo hili litaongeza ushindani ndani ya ligi, litaweka nguvu mpya ya kuchuana kwenye nne bora na moja kwa moja litaendelea kukuza soka la Tanzania kiushindani zaidi.
Fedha kuongezeka
Mapato ya fedha yatokanayo na mechi hizi yanayopelekwa kwa jamii hasa ya wenye uhitaji maalumu yataongezeka maradufu kutokana na wingi wa mechi zenyewe.
Awali, ilikuwa mechi moja pekee, lakini sasa kutapigwa nusu fainali mbili kabla ya fainali lakini pia kutakuwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na kulingana na ukubwa wa timu zinazochuana, kwenye mapato pia kutakuwa na faida kubwa inayotazamiwa kufikiwa kila wakati.