Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Tanzania Prisons, Fred Minziro ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo ili kufikia malengo waliyojipangia.
Maafande hao mipango yao ni kumaliza ligi ndani ya nafasi nne za juu msimu ujao ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya klabu Afrika.
Kocha huyo alieleza kuwa malengo hayo yanaweza kufikiwa lakini kitu cha msingi anahitaji umoja na mshikamano kutoka kwa uongozi, wachezaji pamoja na mashabiki.
“Nataka kuirudisha Prisons ile ya zamani na kutoa upinzani kwenye ligi, hilo linawezekana endapo tutafanya usajili mzuri sababu ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu, tunasikia wenzetu kila siku wanasajili wachezaji wakubwa lakini kama tutajipanga vizuri na tukawa na umoja sidhani kama kuna kitakachotusumbua,” alisema Minziro.
Alisema kwa sasa timu yake imeshaanza mazoezi lakini akiwa na wachezaji walioitumikia timu hiyo kwenye msimu uliopita na baada ya wiki moja anatarajia kuanza kuwapokea wachezaji wapya ambao wamewasajili kwa ajili ya msimu ujao.
Alisema baada ya wachezaji wote kukamilika wanatarajia kwenda Zanzibar au sehemu nyingine ambayo uongozi utaichagua kwenda kupiga kambi kujiandaa na msimu mpya ambao umepangwa kuanza Agosti 15, mwaka huu.
Minziro ametua Prisons akitokea Geita Gold, ambayo aliifundisha kwa mafanikio na kuiwezesha kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 16.
Soka Minziro aomba ushirikiano Prisons
Minziro aomba ushirikiano Prisons
Read also