Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Brazil, Neymar amesema kwamba alilia siku tano mfululizo baada ya Brazil kutolewa kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.
Brazil ilitolewa na Croatia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na baada ya hapo, Neymar alisema kwamba fikra za kustaafu kuichezea timu ya Brazil zilianza kumjia.
Katika mechi hiyo, Neymar aliifungia Brazil bao ambalo iliaminika lingekuwa la ushindi katika dakika za nyongeza lakini Croatia walisawazisha dakika tatu kabla ya mechi kumalizika na hatimaye kuibuka kinara kwenye mikwaju ya penalti na kufuzu hatua ya nusu fainali.
“Siwezi kukwambia nilichokuwa nafikiria kichwani kwangu, ilikuwa ni kama kushindwa kulikoniumiza zaidi katika maisha yangu ya soka, nililia siku tano mfululizo, iliniumiza mno, ndoto zangu ziligeuka na kuwa si chochote,” alisema Neymar.
“Niliona bora nisingefunga lile goli na matokeo kusomeka 0-0 na kisha tupoteze kwenye penalti kuliko kufunga goli ambalo linasawazishwa na tunapoteza kwenye penalti, ni maumivu ambayo ni wachezaji na maofisa wa timu wanaoweza kuelewa,” alisema Neymar.
“Ilikuwa ni tukio baya zaidi katika maisha yangu, ilikuwa ni kama msiba mtu analia upande mmoja na mwingine analia upande wa pili, ilikuwa hovyo, ni hali ambayo sitaki kuipitia kwa mara nyingine,” alisema Neymar.
Neymar ameiwakilisha Brazil kwenye fainali tatu za Kombe la Dunia kuanzia 2014, 2018 na 2022 na baada ya majanga ya fainali za 2022 wazo la kustaafu kuichezea timu hiyo lilimjia lakini sasa amejiwa na fikra mpya na yuko tayari kwa fainali za 2026.