Paris, Ufaransa
Rais wa klabu ya PSG ya Ufaransa, Nasser Al-Khelaifi amepanga kukaa meza moja na mshambuliaji wa timu hiyo, Kylian Mbappe ili kujua hatma yake iwapo anasaini mkataba mpya au anauzwa.
Mbappe ambaye mkataba wake na PSG unafikia ukomo mwakani, aliuandikia barua uongozi wa klabu hiyo akisema hatosaini mkataba mpya lakini angependa aendelee hadi mwakani mkataba wake wa sasa utakapoisha.
Uamuzi huo wa Mbappe umewaweka pagumu mabosi PSG kwani akiendelea kushikilia msimamo huo maana yake ni kwamba mwakani yaani baada ya msimu wa 2023-24 mchezaji huyo atakuwa huru na ataondoka bila ya wao kupata chochote.
Mazingira hayo ndiyo yanayowafanya mabosi PSG kumtaka mchezaji huyo aamue moja kama ni kusaini mkataba mpya wakati huu au auzwe na PSG kupata fedha.
Klabu ya Real Madrid inatajwa kuwa tayari kumnunua mshambuliaji huyo na PSG ipo tayari kufanya biashara wakati huu kama Mbappe ataendelea kushikilia msimamo wake wa kutosaini mkataba mpya.
Al Khelaifi aliwahi kunukuliwa akimtaka Mbappe kuamua moja kama ni kusaini mkataba mpya au kuondoka lakini hawatokubali kuendelea kuwa na mchezaji huyo msimu wa 2023-24 kama hatosaini mkataba mpya.
Baada ya kauli hiyo, Mbappe mwenye umri wa miaka 24 hakujibu chochote hali ambayo huenda ndiyo iliyomfanya Al-Khelaifi kutaka kukaa naye mezani ili kujua moja kama anasaini mkataba mpya au anauzwa.
Kimataifa Rais PSG amtaka Mbappe mezani
Rais PSG amtaka Mbappe mezani
Read also