Na mwandishi wetu
Timu ya Simba leo Ijumaa imemtambulisha kiungo, Fabrice Ngoma baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Ngoma raia wa DR Congo, anakuwa mchezaji wa nne wa kigeni kutambulishwa na timu hiyo kwenye dirisha hili baada ya Muivorycoast, Aubin Kramo na Wacameroon, Che Fondoh Malone na Willy Onana.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema uwezo na uzoefu katika mashindano ya kimataifa ndivyo vitu vilivyowavutia kwa mchezaji huyo ambaye ana historia kubwa katika soka la Afrika.
“Ni mchezaji mkubwa kuwa naye Simba, ni bahati kubwa, zipo timu zilitamani kupata huduma yake msimu ujao lakini zimeshindwa, ameichagua Simba kwa hiyo tunafurahi kwa hilo na tutakuwa naye msimu ujao,” alisema Ally.
Ally alisema bado zoezi hilo linaendelea na kama mambo yatakwenda sawa huenda kesho Jumamosi wakamtambulisha mchezaji mwingine mkubwa baada ya kukamilisha mazungumzo naye na kusaini mkataba wa kuwatumikia Wekundu hao msimu ujao.
Alisema wanachokitaka ni kuona wachezaji hao wanaondoka nchini Julai 17, mwaka huu kuelekea Uturuki kuungana na wenzao kwenye kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu NBC na Mashindano ya Kimataifa.
Ngoma ametua Simba, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Al Hilal ya Sudan aliyojiunga nayo hivi karibuni kutokana na Sudan kukabiliwa na machafuko ya vita.