Na mwandishi wetu
Timu ya Geita Gold imetangaza kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wake mahiri, Elias Maguli,(pichani) utakaomuweka mpaka mwisho wa msimu wa 2023-24.
Maguli aliyetangazwa leo Ijumaa kuongeza mkataba huo ndiye mchezaji wa kwanza wa timu hiyo kuelezwa juu ya kuendelea na timu hiyo msimu ujao baada ya jana Geita kutangaza kutema wachezaji tisa waliomaliza mikataba.
“Timu inaendelea kutengenezwa vizuri zaidi ingawa tayari kuna vitu tumeshavimaliza na tunasubiri muda sahihi ufike tuweke hadharani tuendelee na mengine kwa hiyo Maguli ni mpango wa timu ndiyo maana ameongeza mkataba, tupo naye,” alisema Ofisa Habari wa Geita, Samwel Dida.
Hata hivyo, Wachimba Dhahabu hao tayari wameeleza kumalizana na kocha wao mkuu mpya anayetajwa kutoka nchi za Afrika Mashariki, mabeki wa kati wawili kutoka Kenya na Rwanda, mshambuliaji kutoka Afrika Kusini na wachezaji wengine takriban sita wapya kutoka Tanzania.
Wachezaji walioachana na timu hiyo baada ya kumaliza mikataba ni Danny Lyanga, George Wawa, Mark Arakaza, Geofrey Manyasi, Jonathan Ulaya, Mussa Gadi, Shinobu Sakai, Jonathan Mwaibindi na Juma Luizio aliyeomba kuvunja mkataba.
Soka Maguli aongezewa mwaka Geita
Maguli aongezewa mwaka Geita
Read also