Milan, Italia
Kiungo wa timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu ya Juventus, Paul Pogba (pichani) ametajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa Saudi Arabia akiwa ameandaliwa mkataba wenye thamani ya Pauni 128 milioni.
Gazeti moja linaloandika zaidi habari za michezo nchini Italia lilitoa taarifa hiyo bila kuweka wazi jina la timu inayomtaka mchezaji huyo ingawa inadhaniwa timu zenye nia ya kumsajili kiungo huyo ni kati ya Al Nassr au Al-Ittihad.
Timu hizo mahasimu za jijini Riyadh zinapambana kujiimarisha kwa kusajili wachezaji wenye majina makubwa barani Ulaya na hadi sasa kila moja imefanikiwa kuwasajili mastaa mbalimbali wa Ulaya wakiwamo wachezaji wawili wa zamani wa Real Madrid.
Wachezaji hao mastaa ni Cristiano Ronaldo aliyejiunga na Al-Nassr Januari mwaka huu ingawa alitokea Man United na Karim Benzema ambaye amejiunga na Al-Ittihad mapema mwezi uliopita.
Pogba amekuwa na wakati mgumu Juventus kutokana na kuandamwa na janga la kuwa majeruhi na hivyo kushindwa kuisaidia timu hiyo tangu ajiunge nayo kabla ya msimu uliopita akitokea Man United.
Mchezaji huyo amekuwa na msimu mbaya hadi kushindwa kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar na kufikia tamati Desemba mwaka jana ingawa Ufaransa ilifikia hatua ya fainali kabla ya kubwaga na Argentina waliobeba kombe.
Kwa hali hiyo kabla ya kusajiliwa na klabu yoyote ya Saudi Arabia tatizo la kuwa majeruhi ambalo limemuandama mchezaji huyo ni kati ya mambo yatakayoangaliwa ndipo uamuzi wa kumsajili au kuachana naye ufanyike.
Kimataifa Jina la Pogba laibukia Saudi Arabia
Jina la Pogba laibukia Saudi Arabia
Read also