Na mwandishi wetu
Baada ya kumtwanga Eric Mukadi wa DR Congo, bondia Seleman Kidunda amefunguka akisema kwamba sasa anamtaka bondia yeyote mkali amuoneshe umwamba alionao.
Katika pambano la mabondia hao lililopigwa usiku wa kuamkia leo Jumamosi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Kidunda alimshinda mpinzani wake kwa pointi 99-87, 100-86 na 98-88 baada ya kumaliza raundi zote 10.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa afya mpaka leo na kumaliza pambano langu lakini mpinzani alikuwa mbishi, alijitahidi sababu nilitaka kumaliza kwa K.O raundi ya tatu lakini alijitahidi mpaka mwisho, sasa niseme milango imefunguka nahitaji bondia yeyote yule aje nipambane naye,” alisema Kidunda.
Naye Mukadi alisema: “Mpango wangu ulikuwa mzuri lakini viatu vyangu vilikuwa vikinibana sana ndiyo maana nilikuwa napoteza uwiano, japo mpinzani wangu naye ni mzuri, alikuja kwa kujiamini lakini nilimuonesha ukomavu wa Wacongo mpaka mwisho wa pambano.”
Pambano jingine lililokuwa likisubiriwa kwa hamu ni la Mfaume Mfaume aliyemchapa Chikondi Makawa wa Malawi kwa pointi 79-73, 79-73 na 78-74 katika pambano lililokuwa la raundi nane.