Manchester, England
Kipa wa Man United, David de Gea (pichani) bado hajasaini mkataba na klabu hiyo licha ya mkataba wake wa sasa kufikia ukomo jana Ijumaa na kuwapo matumaini makubwa ya kusaini mkataba mpya.
Awali ilidaiwa kwamba mazungumzo ya kumuongezea mkataba kipa huyo yalifikiwa kabla ya kuwapo mabadiliko katika baadhi ya vipengele vya mkataba mpya baada ya pande zote mbili kufanya tafakuri ya kina.
De Gea mwenye umri wa miaka 32 amekuwa kwenye kikosi cha Man United kwa miaka 12 sasa na amecheza jumla ya mechi 545 na kubeba tuzo kadhaa zikiwamo za kipa bora wa mwaka wa Man United kwa mara nne.
Kocha wa Man United, Erik ten Hag na De Gea kwa nyakati tofauti waliwahi kuzungumzia suala la mkataba huo na kila mmoja kutoa kauli za kujiamini kwamba mkataba mpya ungesainiwa mara baada ya msimu jambo ambalo hadi sasa bado halijafanyika.
Katika hali ya kushangaza De Gea mwenyewe licha ya kuonesha matumaini kwamba angesaini mkataba mpya lakini hadi sasa ameendelea kuwa kimya hali ambayo inaibua hofu kuhusu majaliwa yake ndani ya timu hiyo.
Awali Man United ilidaiwa kumtaka De Gea akubali kupunguziwa mshahara kutoka kiasi anacholipwa cha Pauni 375,000 kwa wiki kwa mujibu wa mkataba aliosaini mwaka 2019.
Na hata ikitokea kupunguziwa mshahara huo, bado atakuwa mmoja wa makipa wanaolipwa fedha nyingi na itakuwa vigumu kupata malipo kama hayo katika klabu nyingine.
Kimataifa De Gea hajasaini mkataba Man United
De Gea hajasaini mkataba Man United
Read also