Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Ibrahim Ajibu amesema kinachowafanya wachezaji washindwe kung’ara wanaposajiliwa na timu kubwa za Simba na Yanga ni woga na kutojiamini.
Ajibu ameeleza hayo ikiwa ni siku moja imepita tangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litangaze kufunguliwa kwa dirisha la usajili kuanzia Julai Mosi mpaka Agosti 31, mwaka huu.
Kiungo huyo aliyewahi kuwika akiwa Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, alisema kinachowavuruga wachezaji wa timu ndogo ni kukutana na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wanapotua kwenye klabu kubwa na kongwe nchini, kitu ambacho mara nyingi humaliza ari walizonazo na kuonekana wamefeli.
“Unajua mchezaji akiwa timu ndogo au ya kawaida anaweza kuonekana lakini anapochukuliwa na kwenda timu kubwa changamoto huwa ni uzoefu wa watu anaokutana nao kikosini na kuingiwa woga, sasa kama wataacha woga na kuanza kupambana wanaweza kucheza na kuwika,” alisema Ajibu.
Alisema anafahamu kundi kubwa la wachezaji wengi wazuri wanaishia njiani wanaposajiliwa na timu kubwa lakini hiyo yote inaweza kuzuilika kama mchezaji atajiamini na kuzizingatia ndoto zake kupitia soka na kipaji alichonacho na si kingine.