Na mwandishi wetu
Tanzania imepanda nafasi saba kutoka ya 130 hadi ya 123 katika viwango vya ubora vilivyotolewa leo Alhamisi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Mara ya mwisho viwango vilivyotolewa Aprili, mwaka huu Tanzania ilikuwa nafasi ya 130, ikitafsiriwa huenda mechi walizocheza hivi karibuni za kufuzu michuano ya Afcon zimeipandisha timu hiyo.
Tanzania iliyoko Kundi F katika michuano hiyo, ilicheza michezo mitatu ambapo kati ya hiyo, ilishinda miwili na kupoteza mmoja.
Michezo hiyo ni dhidi ya Uganda walioshinda ugenini kwa bao 1-0, walishinda dhidi ya Niger nyumbani bao 1-0 na kupoteza nyumbani dhidi ya Uganda kwa bao 1-0.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake ikiwa na pointi saba nyuma ya kinara Algeria yenye pointi 15 huku Uganda ya tatu ikiwa na pointi nne na Niger ya mwisho kwa pointi mbili.
Katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda inashika nafasi ya 92 ikishuka nafasi tatu kutoka ya 89, Rwanda ya 139 ikishuka nafasi nne kutoka 135, Burundi ya 140 ikipanda nafasi tano kutoka 145.
Nchi nyingine za Ethiopia ya 143 ikishuka nafasi moja, Sudan ya 131 ikishuka kutoka 128 wakati DR Congo ni ya 69 ikipanda nafasi moja.
Kwa Afrika, Morocco ni ya 13 ikifuatiwa na Senegal ya 18, Tunisia ikishuka nafasi tatu kutoka ya 28 hadi 31, Algeria ni ya 33 ikipanda nafasi moja, Misri ya 34 ikipanda nafasi moja wakati Nigeria ni ya 39 na Mali ya 50.
Argentina imeendelea kusalia nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Ufaransa, Brazil, England, Ubelgiji, Croatia, Uholanzi, Italia, Ureno na Hispania.
Kimataifa Tanzania yapanda viwango Fifa
Tanzania yapanda viwango Fifa
Read also