Manchester, England
Klabu ya Manchester United imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Chelsea na timu ya Taifa ya England, Mason Mount kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 60 milioni na mkataba wa miaka mitano.
Man United imekuwa ikimuwinda mchezaji huyo katika siku za karibuni na sasa huo unakuwa usajili wa kwanza wa kocha Erik ten Hag katika kipindi hiki cha usajili cha majira ya kiangazi.
Ten Hag kwa sasa anahaha kukiimarisha kikosi chake ili kuhakikisha anafanya vizuri msimu ujao wa 2023-24 kwenye Ligi Kuu England (EPL) pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu uliopita, Chelsea ilitumia Pauni 600 milioni na sasa klabu hiyo inahitajika kuuza baadhi ya wachezaji kabla ya Juni 30 ili kuondokana na hofu ya kubanwa na kanuni za matumizi ya fedha.
Chelsea haikuwa tayari kumuuza kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 lakini imewawia vigumu kusaini naye mkataba mpya hasa kwa kuwa mkataba wake wa sasa unafikia ukomo mwakani hivyo ingeweza kumuacha akaondoka bila ya wao kupata chochote.
Tayari Chelsea imeshawapiga bei Kai Havert katika klabu ya Arsenal na Mateo Kovacic aliyetua Man City wakati kipa Edouard Mendy, Kalidou Koulibaly na N’Golo Kante wameuzwa katika klabu za Al-Ahli na Al-Ittihad za Saudi Arabia.
Mount (pichani juu) ameifungia Chelsea mabao 33 katika mechi 195 za Chelsea tangu ajiunge na kikosi cha kwanza cha timu hiyo mwaka 2019, msimu huu umekuwa mgumu kwake kutokana na kuandamwa na majeraha lakini kwa ujumla Chelsea nayo haikuwa na msimu mzuri, imemaliza EPL ikiwa nafasi ya 12.
Mount alishiriki kikamilifu katika timu ya Chelsea iliyotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021 waikiibwaga Man City kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali ambayo Mount alikuwamo kwenye kikosi cha kwanza.
Kimataifa Man United yamnasa Mason Mount
Man United yamnasa Mason Mount
Read also