Riyadh, Saudi Arabia
Kipa wa timu ya Taifa ya Senegal, Edouard Mendy (pichani) ameachana na klabu ya Chelsea na kujiunga na klabu ya Al-Ahli ya Saudi Arabia.
Mendy ni mchezaji mwingine wa Chelsea aliyehamia Saudi Arabia akiwa ametanguliwa na wachezaji wenzake aliokuwa nao Chelsea, Kalidou Koulibaly na N’Golo Kante.
Akiwa Chelsea, Mendy amefanikiwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2020-21 ambapo pia alitwaa tuzo ya kipa wa msimu wa Uefa na kipa bora wa Fifa kwa mwaka 2021.
Mendy alijiunga na Chelsea mwaka 2020 akitokea klabu ya Rennes ya Ufaransa na alikuwamo katika kikosi cha Senegal kilichobeba taji la Mataifa ya Afrika wakiitoa Misri kwa mikwaju ya penalti huku Mendy akiibuka shujaa katika hatua hiyo.
Kipa hiyo hata hivyo tangu Septemba mwaka jana alijikuta katika wakati mgumu kwenye kikosi cha Chelsea baada ya kocha Thomas Tuchel kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Graham Potter.
Tangu Potter awe kocha, Mendy ameishia kucheza mechi tatu tu na wakati wote alikuwa kipa namba mbili huku Kepa Arrizabalaga akiwa chaguo la kwanza kwa Potter.
Katika taarifa ya kumuaga Mendy, klabu ya Chelsea imemtaja kuwa alikuwa mchezaji mwenye tabia nzuri ndani na nje ya uwanja na wakati wote ataendelea kuwa na nafasi yake katika historia ya klabu ya Chelsea hasa kwa mchango wake hadi timu hiyo kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021.
Wachezaji wengine mastaa wa Ulaya waliotimkia Saudi Arabia hivi karibuni ni Ruben Neves na Karim Benzema waliotangualiwa na Cristiano Ronaldo hapo hapo zipo habari kwamba winga wa Chelsea, Hakim Ziyech naye yuko mbioni kuelekea Saudi Arabia.
Kimataifa Mendy naye atimkia Saudi Arabia
Mendy naye atimkia Saudi Arabia
Read also