Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Ihefu, umesema hauna mpango wa kubadili benchi lao la ufundi kutokana na mafanikio waliyowapata msimu uliopita.
Ihefu maarufu kama Mbogo Maji, msimu uliopita ilimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi 39.
Katibu Mkuu wa Ihefu, Athuman Mndolwa alisema kuwa wameridhishwa na utendaji wa makocha wao, Zuberi Katwila na John Simkoko (pichani) na watakachokifanya ni kuongeza wachezaji watatu ili kuziba nafasi ambazo zilionesha mapungufu msimu uliopita.
“Malengo yetu msimu unaokuja ni kumaliza ndani ya tano bora na hiyo inatokana na ubora wa benchi letu la ufundi ambalo tumeridhishwa na utendaji wao na tutaendelea nalo msimu ujao lakini pia tumepanga kuwaongezea wachezaji wengine watatu ili kukiimarisha kikosi chetu,” alisema Mndolwa.
Kiongozi huyo alisema pamoja na kuanza vibaya ligi ya msimu uliopita lakini walikuwa na imani na ubora wa kikosi chao na hilo limeonekana baada ya wachezaji kuzoeana na baadae kufanya vizuri.
Alisema pia, wamepanga kubakisha asilimia kubwa ya wachezaji wao waliokuwepo msimu uliopita ili kuendeleza kiwango walichokionesha mwishoni mwa msimu uliopita wa 2022-23 na kufikia malengo yao ya kumaliza msimu ujao ndani ya tano bora.
Ihefu ni miongoni mwa timu mbili zilizochukua pointi tatu mbele ya mabingwa watetezi Yanga ikiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Highland Estate, Mbeya.
Soka Ihefu kutobadili makocha
Ihefu kutobadili makocha
Read also