Na Hassan Kingu
Simba imeachana na kiungo Jonas Mkude ambaye mbali na mashabiki kutaka kujua timu mpya atakayojiunga nayo lakini pia amewaachia kumbukumbu zilizogawanyika katika sura mbili.
Sura ya kwanza ya Mkude ni ile ya kiungo mahiri na mwenye uwezo ambaye kila shabiki wa Simba na hata Taifa Stars alifurahi kumuona akiwa amevaa jezi mojawapo ya timu hizo.
Kwa kipindi kirefu ambacho amekuwa Simba, Mkude au Nungunungu ameishi katika umahiri huo kiasi cha kumfanya awe kipenzi cha mashabiki kila mara anapokuwa uwanjani akiiwakilisha timu hiyo.
Mkude ana matukio mengi yaliyodhihirisha ubora wake lakini kwa harakaharaka umahiri wake ambao unaweza kukumbukwa zaidi na mashabiki wengi wa Simba au hata Yanga ni katika mechi ya Kariakoo Derby au Dar Derby, ni siku ambayo Mkude na Feisal Salum au Fei Toto waliteka nyoyo za mashabiki.
Kama mashabiki waliufurahia mpambano na Fiston Mayele na Joash Onyango au Mayele na Henock Inong basi mpambano mwingine wa kuvutia na kukumbukwa katika mechi hiyo ni wa Fei Toto na Mkude.
Mkude na Fei Toto kila mmoja alifanikiwa kuonesha uwezo wake katika kulitawala dimba la kati na kubwa zaidi waliinogesha mechi hiyo na kuwa na mvuto, waliwafurahisha mashabiki, waliipa hadhi Dar Derby, hadhi ambayo mashabiki wanaiihitaji.
Huko nyuma haikuwa ajabu kusikia Mkude yumo kwenye kikosi cha Stars, ubora na sifa anazotakiwa kuwa nazo mchezaji mahiri, alikuwa nazo Mkude, ni aina ya mchezaji ambaye angeweza kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu yoyote ile Afrika.
Hiyo ndiyo sura ya kwanza ya Mkude, ambayo mashabiki hasa wa Simba wataendelea kumkumbuka wakati huo huo wakijiuliza nini hasa kimemkuta hadi akawa si tena mchezaji wa kikosi cha kwanza, si tena mchezaji anayeaminiwa kwenye mechi kubwa za Simba ikiwamo Dar Derby.
Si mchezaji ambaye unaweza kusema msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Simba hadi kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hapo hapo ndipo tunapoipata sura ya pili ya Mkude, sura ya mchezaji wa kiungo ambaye amepoteza au amekubali kupoteza umahiri na ubora uliomfanya awe kipenzi cha mashabiki wa Simba, amepoteza hadhi aliyokuwa nayo.
Mkude ambaye ilikuwa panga pangua hakosekani kikosi cha kwanza taratibu akageuka na kuwa si tu mchezaji wa kusugua benchi bali wakati mwingine anakosekana hata katika wachezaji wa akiba.
Si Mkude ambaye ungetegemea kwenye Dar Derby apambane na Fei Toto au aisumbue safu ya kiungo ya Yanga, badala yake amekuwa Mkude mwingine ambaye hatimaye Simba imeamua kuachana naye.
Kwa sasa Mkude si tu hana nafasi Simba bali inaweza kuonekana ajabu jina lake likiwemo kwenye kikosi cha Stars, huko nyuma kukosekana kwa Mkude kungeacha maswali lakini leo hakuna maswali.
Katika sura ya pili ya Mkude kuna swali linalokuja kwamba nini hasa kimemkuta, je kashuka kiwango hadi kushindwa kupigania namba katika kikosi cha Simba kilichosheheni mastaa kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika?

Je walichoweza kina Aboubakar Salum, Mudathir Yahya na Fei Toto na wengineo katika Yanga ndicho kilichomshinda Mkude hadi akajikuta hapati nafasi Simba na hatimaye akajikuta akiachwa?
Sura ya pili ya Mkude inamfikirisha kila shabiki na kuacha maswali, je ni kweli ameshuka kiwango au ni ile hadithi inayosikika kwamba si mtu mchezaji mwenye nidhamu, kwamba pamoja na uwezo wake wote tatizo la nidhamu limekuwa likimsumbua. Je ni kweli tatizo ni nidhamu pekee au kiwango kimeshuka?
Jibu la swali hili huenda likapatikana msimu ujao katika timu ambayo itamsajili Mkude, kama ni Yanga, Azam au kwingineko hapa hapa Tanzania au ataamua kuvuka mipaka ya nchi.
Yote kwa yote mashabiki walio wengi bado wanaitamani sura ya kwanza ya Mkude yaani Mkude au Nungunungu, kiungo mahiri ambaye hawajui nini hasa kimemkuta, ameshuka kiwango au ana tatizo jingine nje ya hilo?