Na mwandishi wetu
Kipa wa Taifa Stars, Beno Kakolanya (pichani) hatimaye ameweka wazi kuwa ameondoka katika klabu ya Simba baada ya kushindwana kwenye dau la usajili kwa ajili ya mkataba mpya.
Beno amezungumza hayo leo alipokuwa akihojiwa na redio ya EFM akifafanua kuwa alizungumza na uongozi wa Simba ili kuongeza mkataba mpya lakini walishindwana baada ya ofa ambayo hakuitaja, kutofika alipokuwa anatarajia.
Kipa huyo wa zamani wa Yanga alisema baada ya kumalizana na Simba alipata ofa nyingine ya timu iliyokuwa ikimuhitaji Saudi Arabia inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza lakini wakati hayo yakiendelea iliibuka timu nyingine iliyomuwekea ofa kubwa mezani.
“Timu niliyokuwa nacheza (Simba) niliwapa nafasi kwanza, walinipa ofa lakini haikufika nilipohitaji, siwezi kuzungumzia kuhusu mtazamo wao kuhusu ofa waliyonipa lakini kwangu nilijiangalia umri na maslahi yangu nilihitaji zaidi na mwisho hatukuafikiana.
“Nilipata ofa nyingine pia moja ya timu inacheza Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia lakini napo pia kuna mwingine akaja kutoka hapa hapa nyumbani na ofa yao ikawa kubwa kuliko, ikawa hivyo,” alisema Kakolanya bila ya kutaja timu hiyo ya mwisho iliyomletea ofa nono zaidi.
Kakolanya ambaye anakiri kujivunia kushiriki michuano ya klabu Afrika akiwa na timu hiyo hata hivyo zipo habari kwamba ameshamalizana na timu ya Singida Fountain Gate.
Singida ambayo inatarajia kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ipo kwenye harakati za kuiboresha timu hiyo kwa ajili ya kufanya vyema katika michuano hiyo na Ligi Kuu NBC wakishiriki kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kupanda daraja msimu uliopita.