
Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa klabu ya PSG na timu ya Taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesema kwamba ana sifa zote za kuwa mmoja wa wateule wa kushinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2023.
Mbappe ambaye jana Jumatatu alifunga bao pekee la Ufaransa dhidi ya Ugiriki ana rekodi ya kufunga mabao 54 kwa msimu mmoja kwenye klabu na timu ya Taifa akivunja rekodi ya Just Fontaine ya msimu wa 1957-58.
Katika klabu msimu huu wa 2022-23, Mbappe ameisaidia PSG kushinda taji la Ligi 1 na ameonyesha umahiri kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa kushinda kiatu cha dhahabu akipiga hat trick katika mechi ya fainali dhidi ya Argentina ambao ndio walioibuka vinara.
Alipoulizwa kama anafaa kufikiriwa katika tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu, Mbappe hakuwa na jibu la moja kwa moja ingawa alijitaja kwamba ana sifa zote stahiki.
“Wakati wote ni vigumu kuizungumzia tuzo ya mtu mmoja kwa sababu ni lazima ujiweke mbele kwa namna yako na hilo ni jambo ambalo umma haulikubali, kigezo kipya kinahusu mtu mwenye mchango mkubwa, nafikiri nipo katika hilo, kwa hiyo naweza kusema ndio nastahiki lakini ngoja tuone,” alisema Mbappe.
Katika Ballon d’Or msimu huu, Mbappe atachuana na mchezaji mwenzake wa zamani wa PSG Lionel Messi ambaye amejiunga na Miami FC ya Marekani, pia atachuana na Erling Haaland wa Man City.
Messi ndiye aliyekuwa mchezaji bora katika fainali za Kombe la Dunia 2022 na ndiye aliyeiwezesha nchi yake kubeba taji hilo wakati Haaland kamaliza msimu wake wa kwanza Man City na mabao 52 na kuiwezesha timu hiyo kuweka rekodi kwa kubeba mataji matatu katika msimu mmoja.