Na waandishi wetu
Taifa Stars leo Jumapili imeichapa Niger bao 1-0 katika mechi ya Kundi F ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na kujiimarisha katika nafasi ya pili baada ya Uganda Cranes kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Algeria.
Kwa ushindi huo Stars inakuwa imefikisha pointi saba ikiwa nafasi ya pili nyuma ya kinara wa kundi hilo Algeria yenye pointi 15, Cranes inabaki nafasi ya tatu na pointi nne na Niger ipo mkiani ikiwa na pointi zake mbili.
Timu zote za kundi hilo kila moja imecheza mechi tano na kila moja imebakisha mechi moja itakayopigwa baadaye mwezi Septemba na kutoa hatma ya timu ipi itakayomaliza nafasi ya pili nyuma ya Algeria kati ya Stars na Cranes.
Katika mechi zijazo Stars itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Algeria, ambazo zitaumana huku Stars ikitambua ugumu uliopo kwenye kundi lake licha ya kuwa nafasi ya pili lakini Cranes walio nafasi ya tatu nao mechi ya mwisho ina maana kubwa kwao. Stars na Cranes zote kila moja ina mabao matatu ya kufunga, kila moja ina sare moja, tofauti ya timu hizo ni katika mechi za kupoteza, Stars imepoteza mbili wakati Cranes imepoteza tatu.
Kwa mantiki hiyo mechi zijazo zitakuwa kama mtihani utakaokuja na jibu la timu ipi itakayoshinda na aina ya ushindi kwani idadi ya mabao na mechi za kupoteza ni vitu vitakavyokuwa na maana kubwa katika mechi hizo.
Katika mechi ya Stars iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam timu hiyo ilineemeka kwa bao hilo pekee la Simon Msuva katika dakika ya 69 akiutumia mpira uliopigwa na Novatus Ibrahim.
Katika mechi ya Cranes iliyopigwa kwenye Uwanja wa Japoma mjini Douala, Cameroon, mabao ya washindi yote yalifungwa na Mohamed Amoura dakika za 42 na 66 wakati bao pekee la Cranes lilifungwa na Fahd Bayo dakika ya 88.
Algeria hadi sasa hawajapoteza hata mechi moja na wameshafuzu kushiriki fainali za michuano hiyo zitakazopigwa mwakani nchini Ivory Coast, watacheza mechi ya mwisho ya kundi hilo kukamilisha ratiba kama ambavyo Niger nao watacheza kukamilisha ratiba dhidi ya Cranes wanaowania kuishusha Stars na hivyo wataombea Stars ipoteze kwa Algeria na wao waishinde Niger kwa mabao mengi..
Kimataifa Stars yaitambia Niger, Uganda Cranes hoi
Stars yaitambia Niger, Uganda Cranes hoi
Read also