Na mwandishi wetu
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi ameeleza huzuni yake kuondoka katika klabu hiyo, akisema hakufanya maamuzi hayo kwa ajili ya fungu la pesa alilowekewa na klabu anayojiunga nayo.
Juzi Jumatano, Yanga ilitangaza kuachana na Nabi raia wa Tunisia baada ya kocha huyo kutotaka kuongeza mkataba na kuhitaji changamoto mpya.
Nabi ambaye anahusishwa kuhamia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza pia namna gani anamshukuru mfadhili wa Yanga, Ghalib Said, wachezaji, benchi la ufundi, mashabiki kwa ushirikiano waliompa tangu ametua Yanga.
“Ni jambo gumu zaidi nimelazimika kufanya katika miaka miwili iliyopita, lakini mambo yote mazuri lazima yafike mwisho. Tulipitia mihemko yote pamoja, huzuni, furaha, wakati mwingine hasira, lakini kwa neema ya Mungu tuliishi nyakati zisizosahaulika,” aliandika Nabi.
Kocha huyo ameshukuru pia kufanikisha mengi ambayo wengi hawakutarajia kutoka kwake wakati anatua Yanga miaka miwili na nusu iliyopita lakini kwa walipofikia, anawashukuru mno wachezaji wake ambao aliwachukulia kama watoto wake na kufanikisha mafanikio waliyoyapata mpaka sasa.
Pia, amewashukuru kamati ya utendaji, watendaji wenzake wa benchi la ufundi akibainisha bila wao hakuna ambacho kingewezekana huku akibainisha namna anavyowapenda mashabiki wa Yanga kwa nguvu na ujasiri waliompa wakati wote.
“Hatimaye, mashabiki, hakuna maneno yanayoweza kuelezea kiwango cha upendo nilichonacho kwenu na nguvu zote mlizonipa. Naumia moyoni kuachana nanyi, lakini ndivyo maisha ya ukocha yalivyo.
“Ningependa kuwaambia, haijawahi kuwa juu ya pesa, na kwamba muumini mzuri anajua kuwa pesa tunayopata katika maisha yetu tayari imepangwa kwa ajili yetu na kwamba kupata pesa hizo leo au kesho haitabadilika. Kwaheri familia yangu, nitawakumbuka sana. Nawapenda wote,” aliandika Nabi.
Nabi aliyetua Yanga akitokea Al Merrikh ya Sudan, anaondoka akiwa ameipa Yanga mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, mataji mawili ya Kombe la FA, mataji mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha Yanga kwa mara ya kwanza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.