Madrid, Hispania
Kiungo mpya wa Real Madrid, Jude Bellingham amesema kwamba angependa kuona mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe akiungana naye katika timu hiyo.
Bellingham mwenye umri wa miaka 19 ametoa kauli hiyo leo Alhamisi mara baada ya kutambulishwa rasmi na klabu hiyo kwenye uwanja wa mazoezi akiwa tayari amesaini mkataba wa miaka sita.
Mchezaji huyo alikabidhiwa jezi namba 5 ambayo miaka ya nyuma ilikuwa ikivaliwa ba Zinedine Zidane, kiungo nyota wa zamani wa timu hiyo ambaye Bellingham alikuwa akivutiwa na soka lake.
Katika tukio la utambulisho huo, rais wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez alimtaja Bellingham kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani kabla ya mchezaji huyo kuulizwa maswali na waandishi wa habari.
Bellingham ambaye pia aliwahi kuichezea Birmingham City kabla ya kujiunga na Borussia Dortmund ya Ujerumani alisema kwamba asingeweza kuzungumzia lolote kuhusu mpango wa Mbappe na Real Madrid.
“Ni mchezaji mzuri chochote atakachoamua kufanya namtakia heri, je ningependa kucheza na mchezaji wa aina ya Mbape? Nani ambaye hangetaka,” alisema Bellingham.
“Sababu hasa ya kunifanya niseme hii ni siku kubwa pekee ya kujivunia katika maisha yangu ni kwa sababu hii ni klabu kubwa ya soka katika historia ya mchezo huu, si wachezaji wengi wanaopata nafasi ya kucheza katika klabu hii yenye historia ya kipekee, hakika naona ufahari,” alisema Bellingham.

Hadi kumnasa Bellingham, Real Madrid imezibwaga klabu za Manchester City na Liverpool ambazo zote zilionesha nia ya kumtaka mchezaji huyo wa England ambaye pia aling’ara na timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia Desemba mwaka jana.
Akipinga hoja ya pesa kuwa kishawishi cha yeye kuamua kujiunga na Real Madrid, Bellingham alisema alipewa ruhusa na Dortmund na kuzungumza na maofisa wa Real Madrid na akavutiwa na hilo na si kwa sababu timu nyingine ni mbaya bali Madrid ni timu kubwa.
Alisema wakati wote alifahamu kutakiwa na timu za England na hilo kwake lilikuwa jambo la kawaida, lakini alishangaa na kushtuka alipotajiwa kutakiwa na Real Madrid.
“Nilishtuka na kupigwa na bumbuwazi kidogo baba aliponikalisha chini na kuniambia unatakiwa na Real Madrid, ilikuwa kama vile mapigo ya moyo yanataka kusimama, ni jambo ambalo hulitarajii kuwapo, hufikirii kwamba kuna siku utaichezea timu kama hii,” alisema Bellingham.
Real Madrid pia imemsajili beki wa kushoto, Fran Garcia na kiungo Brahim Diaz wakati ikijipanga kwa ajili ya msimu wa 2023-24 ili kulipigania na kulibeba taji la La Liga ambalo limebebwa na Barcelona lakini pia inapigania taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo limebebwa na Man City.
Klabu hiyo pia inatafuta mshambuliaji baada ya kuondoka kwa Karim Benzema aliyejiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia, washambuliaji ambao wapo kwenye rada zao ni Mbape wa PSG na Harry Kane wa Tottenham.
Bellingham hata hivyo hakutaka kumzungumzia Kane ambaye pia ni mchezaji mwenzake wa timu ya Taifa ya England. “Kuhusu Kane na uvumi uliopo siwezi kusema lolote, ni mchezaji wa hadhi ya juu duniani, ni nahodha wangu, nampenda kama binadamu, chochote kitakachotokea acha kitokee.”
Bellingham anakuwa mchezaji wa sita wa England kusajiliwa Real Madrid akiwa ametanguliwa na kina Laurie Cunningham, Steve McManaman, David Beckham, Michael Owen na Jonathan Woodgate.
Kuhusu Zidane ambaye Bellingham amekabidhiwa namba yake alisema, “Nimekuwa nikisema katika mahojiano mara nyingi kwamba navutiwa na Zinedine Zidane, sitaki kujaribu kuwa kama yeye badala yake najaribu kuwa Jude lakini ni wazi kwamba alikuwa bora.