Na mwandishi wetu
Taasisi ya Fountain Gate imeinunua timu ya Singida Big Stars inayoshiriki Ligi Kuu NBC na sasa rasmi itajulikana kama Singida Fountain Gate FC na makazi yao yataendelea kuwa mkoani Singida.
Singida BS wamemaliza msimu wa Ligi Kuu NBC 2022/23 katika nafasi ya nne wakifikisha pointi 55 na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupanda kushiriki ligi kuu msimu huu.
Hii inakuwa mara ya tatu kwa timu hiyo kubadili majina, awali wakati inashiriki Championship ilikuwa ikiitwa DTB, ilipopanda ligi kuu ikaitwa Singida BS na sasa itaitwa Singida Fountain Gate FC.
Safu mpya ya Singida Fountain Gate FC iliyotangazwa jana itakuwa chini ya Rais Japhet Makau ambaye atakuwa na wajumbe wanane; Festo Sanga, Musa Sima, Joseph Msafiri ambaye pia ni mkuu wa shule za Fountain Gate Academy.
Wajumbe wengine ni Alexander Mnyeti aliyekuwa mmliki wa zamani wa timu ya Gwambina, Ibrahim Mirambo, Omar Kiwanda na John Kadutu ambaye ni mtendaji mkuu na mjumbe wa kamati ya sheria na hadhi za wachezaji.
Akizungumza leo Jumatano jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi za Fountain Gate Academy Tanzania, Japhet Makau alisema kuchukua timu hiyo itatoa fursa kwa vijana kuonekana kwa sababu taasisi hiyo ina timu za Fountain Gate FC na Fountain Gate Princess zinazocheza ligi inayotambulika na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Kupata timu ya Singida Fountain Gate katika ligi itawapa nafasi wachezaji kutoka katika kituo chao na timu kutoka Ligi Daraja la Kwanza kupata nafasi ya kucheza ligi kuu na kucheza michuano ya kimataifa.
“Tumenunua timu hiyo na itaendelea kubaki Singida, kwa kuwa Singida Fountain Gate FC inashiriki michuano ya kimataifa na Caf (Shirikisho la Soka Afrika) wanahitaji timu zote zinazoshiriki michuano hiyo kumiliki timu ya wanawake hali hiyo inatulazimimu timu yetu ya wanawake ya Fountain Gate Princess kuwa mali ya Singida Fountain Gate FC,” alisema Makau.