Na mwandishi wetu
Licha ya KMC kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Mbeya City jana, kocha mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema bado wana imani ya kupindua matokeo kwenye mchezo wa marudiano.
KMC ilipokea kipigo hicho kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuwania kutoshuka daraja na kuendelea kushiriki Ligi Kuu NBC msimu ujao. Mechi ya marudiano itapigwa Dar es Salaam Juni 16, mwaka huu.
Julio alisema anawapongeza vijana wake kwa kupambana kutafuta ushindi lakini walifungwa na kwa matokeo hayo yanampa matumaini ya kupata ushindi kwenye mchezo wa pili na kusalia ligi kuu.
“Mechi hizi ni ngumu sababu wote tunataka kujinusuru na kusalia ligi kuu, nimekubali tumefungwa na goli moja tulilolipata tutalitumia vizuri kutafuta faida kubwa tukiwa nyumbani. Vijana wamepambana, wameonesha kuna jambo wanalitafuta na sasa tunakwenda kujipanga vizuri nyumbani,” alisema Julio.
Naye Kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru alisema: “Tulikuwa na nafasi ya kufunga mabao mengi lakini imeshindikana, kikubwa tumepata ushindi na sasa tunajipanga kuhakikisha tunaulinda ushindi wetu na kutafuta matokeo mazuri zaidi.”