Istanbul, Uturuki
Rais wa klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa, Nasser Al-Khelaifi amesema hahusiki kwa namna yoyote katika mpango wa Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani kuinunua klabu ya Manchester United.
Al-Khelaifi (pichani) japo amekiri kwamba mpango wa kuinunua klabu hiyo unafanywa na Sheikh Jassim ambaye ni raia mwenzake wa Qatar lakini yeye hahusiki kwa namna yoyote katika mpango huo.
“Paris Saint-Germain ndio klabu yangu, ipo ndani ya moyo wangu na haihusiani kwa namna yoyote na Man United,” alisema Al-Khelaifi akielezea tofauti ya Man United na PSG.
Kauli ya Al-Khelaifi imekuja baada ya Ijumaa iliyopita kuwapo habari kwamba alifanya kazi kubwa katika mazungumzo ili kuhakikisha Sheikh Jassim anatimiza azma yake ya kuinunua Man United kutoka Familia ya Glazer.
Al-Khelaifi ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Asia, alisema mwekezaji yeyote huwa anatafuta ushauri na yeye anakuwa tayari kutoa ushauri kuhusu Man United au klabu yoyote.
Wiki iliyopita, Sheikh Jassim aliwasilisha ofa yake ya kutaka kuinunua Man United kwa mara ya tano lakini hadi sasa ofa hiyo bado ipo mezani na haijulikani kama atafanikiwa au la licha ya kwamba anaonekana amepania kuinunua klabu hiyo.
Wakati huo huo, Familia ya Glazer pia inatafakari maombi ya bilionea wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe ambaye naye anaitaka klabu hiyo pamoja na wawekezaji wengine kutoka nchini Marekani.
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) lina kanuni inayokataza wamiliki au wafanyabiashara kuwa na nguvu kwenye klabu zaidi ya moja kushiriki katika mashindano ya Ulaya.
Sheria hiyo iliyopitishwa miaka 25 iliyopita lengo lake ni kulinda hadhi na heshima ya mchezo wa soka kutoka kwa wamiliki ambao wanaweza kuwa na maslahi binafsi katika timu husika.