Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu NBC wakati kocha wake Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amechaguliwa kuwa kocha bora.
Uteuzi wa wawili hao umetangazwa leo Jumapili kupitia taarifa ya Idara ya Habari, Mawasiliano ya TFF ikiwa ni siku moja kabla ya kutolewa kwa tuzo za jumla za wachezaji wa ligi hiyo msimu wa 2022-23.
Katika tuzo hizo za jumla ambazo hafla yake itafanyika mkoani Tanga mara baada ya mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Azam, Ntibazonkiza pia anawania tuzo ya mfungaji bora akiwa amefungana idadi ya mabao na Fiston Mayele wa Yanga.
Wachezaji hao kila mmoja amezifumania nyavu mara 17 na mjadala uliopo sasa miongoni mwa wadau wa soka nchini ni kama TFF itawapa wachezaji hao wawili tuzo hiyo au itakuwa na kigezo cha kumpa mmoja.
Ntibazonkiza ametwaa tuzo ya mwezi Mei akibebwa na mabao saba aliyofunga katika mechi mbili, alifunga mabao mawili katika mechi na Coastal Union katika ushindi wa 3-1, akafunga mabao matano katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania.
Katika kipindi hicho hicho cha mwezi Mei, Ntibazonkiza pia alihusika katika mabao mawili ya Simba na hivyo kuwashinda Prince Dube wa Azam na Charles Ilamfya wa Mtibwa Sugar aliokuwa akichuana nao.
Kwa upande wa Robertinho ametwaa tuzo hiyo akibebwa na ushindi wa timu yake wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting, 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania, 3-1 dhidi ya Coastal Union na sare ya bao 1-1 na Namungo.
Katika kuwania tuzo ya kocha bora, Robertinho aliwabwaga makocha wenzake Melis Medo wa Dodoma Jiji na Daniel Cadera wa Azam FC.
Naye meneja wa Uwanja wa Azam Complex wa Chamazi jijini Dar es Salaam, Amir Juma ametwaa tuzo ya meneja bora wa uwanja kwa mwezi Mei baada ya kufanya vizuri katika usimamizi wa matukio ya michezo pamoja na ubora wa miundombinu.
Soka Ntibazonkiza mchezaji bora mwezi Mei
Ntibazonkiza mchezaji bora mwezi Mei
Read also