Barcelona, Hispania
Uamuzi wa Lionel Messi kujiunga na Inter Miami FC ya Marekani unaonekana kuwakera Barca ambao walipania kumrudisha mchezaji huyo ili amalizie maisha yake ya soka la ushindani na timu hiyo.
Na ingawa habari za ndani zinadai kwamba Barca inabanwa na kanuni za La Liga za matumizi ya fedha katika usajili wa Messi lakini uamuzi wa mchezaji huyo kwenda Marekani haujawafurahisha.
“Jumatatu Jorge Messi, baba mzazi wa mchezaji na mwakilishi wake alimuarifu rais wa klabu Joan Laporta kuhusu uamuzi wa mchezaji huyo kuhamia Inter Miami,” ilieleza taarifa ya Barca.
“Hii ni mbali na ukweli kwamba waliwasilishiwa ombi na klabu kwa kuzingatia shauku iliyokuwapo ya Barcelona na Messi kwa mara nyingine kuvaa jezi ya klabu hiyo,” ilifafanua taarifa hiyo.
“Rais Laporta ameelewa na kuheshimu uamuzi wa Messi kutaka kwenda kwenye ligi isiyo na mahitaji mengi, kujiweka mbali na kuepuka kufuatiliwa pamoja na presha ambayo amekuwa akikutana nayo katika miaka ya karibuni,” ilieleza taraifa hyo.
Messi ambaye mkataba na klabu ya PSG ya Ufaransa unafikia ukomo Juni 30 mwaka huu alikuwa akihusishwa na mipango ya kurudi timu yake ya zamani ya Barca lakini jambo hilo limeshindikana baada ya Messi mwenyewe kuichagua Inter Miami kwa kile alichoeleza kwamba asingependa kujikuta katika mazingira aliyokutana nayo mwaka 2021 hadi akalazimika kujiunga na PSG.
Barca ililazimika kumruhusu Messi kujiunga PSG baada ya kubanwa na kanuni za usajili chanzo kikiwa ni matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria za La Liga.
Kocha wa Barca, Xavi Hernandez, ambaye amewahi kucheza na Messi wakiwa Barca ndiye aliyeongoza harakati za kumshawishi mchezaji huyo kurudi katika klabu hiyo anaye lisema kwamba anaheshimu uamuzi wa Messi.
“Tumezungumza naye sana na nimebaini mabadiliko katika siku za karibuni, labda hakuona kilichoendelea, tunalazimika kuheshimu uamuzi wake,” alisema Xavi.
Messi, mshindi wa Ballon d’Or mara saba na ambaye baadaye mwezi huu atafikisha miaka 36 pia alikuwa akitajwa katika mpango wa kwenda Saudi Arabia kujiunga na klabu ya Al-Hilal ya huko lakini hatimaye ameamua kwenda kucheza soka Marekani akiziacha Barca na Al-Hilal.
Akiwa Marekani Messi huenda akaungana na nyota mwingine wa zamani wa Barca, Sergio Busquets kwani naye kwa sasa yuko katika mazungumzo na Inter Miami FC.