Prague, Jamhuri ya Czech
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 43, West Ham United imetwaa taji la kwanza lenye hadhi jana Jumatano ilipoilaza Fiorentina mabao 2-1 na kutawazwa vinara wa michuano ya Europa Conference Ligi.
Mara ya mwisho West Ham kubeba taji ilikuwa mwaka 1980 ilipobeba Kombe la FA na kwa Ulaya ilibeba taji la mwisho mwaka 1965, Kombe la Washindi Ulaya.
Nahodha wa West Ham, Declan Rice ambaye hapana shaka hiyo ilikuwa mechi yake ya mwisho na timu hiyo kwani amekuwa akiwindwa na klabu kadhaa na ameonesha nia ya kutaka kuhama, atakuwa amewaaga mashabiki wa timu hiyo akiwa hana deni nao.
Kwa kuweka rekodi sawa, Rice anakuwa nahodha wa tatu wa timu hiyo kubeba kombe akitanguliwa na Bobby Moore mwaka 1965 (Kombe la Washindi Ulaya) na Billy Bonds mwaka 1975 na 1980 (Kombe la FA).
Mtu mwingine ambaye ushindi wa West Ham lilikuwa tukio la kipekee kwake ni kocha wa timu hiyo, David Moyes ambaye mara baada ya kukabidhiwa medali ya ushindi na Rais wa Uefa, Aleksander Ceferin alikwenda nayo moja kwa moja hadi sehemu aliyokuwa baba yake.
Moyes ambaye ana miaka 60, kwanza alimkumbatia mzazi wake huyo mwenye umri wa miaka 87 kabla ya kumvalisha medali aliyokabidhiwa na kisha wawili hao wakaangaliana usoni kwa muda mfupi wote wakiwa katika hali ya furaha.
Ushindi huo hata hivyo uliandamana na majanga baada ya baadhi ya mashabiki kufanya fujo ambapo mchezaji wa Fiorentina, Cristiano Biraghi aliumizwa kichwani kiasi cha kutokwa na damu.
Mchezaji huyo inaaminika aliumia baada ya kurushiwa kitu ambacho hakikuweza kufahamika mara moja wakati ambao baadhi ya mashabiki walianza kurusha chupa za maji na vinywaji uwanjani.
Katika mechi hiyo West Ham ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Benrahma kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 62 lakini Fiorentina inayoshiriki Ligi ya Serie A Italia, ilisawazisha dakika tano baadaye kwa bao lililofungwa na Bonaventura.
Wakati kukiwa na matarajio ya timu kwenda kwenye dakika za nyongeza, Jarred Bowen aliipatia West Ham bao la ushindi katika dakika ya 90, bao lililotosha kuifanya West Ham iandike historia mpya.
Kwa kubeba taji hilo ambalo msimu uliopita lilibebwa na AS Roma ya Italia, West Ham inayoshriki Ligi Kuu England, imejihakikishia nafasi ya kushiriki Europa Ligi msimu ujao.
Kimataifa West Ham vijogoo Europa Conference
West Ham vijogoo Europa Conference
Related posts
Read also