Madrid, Hispania
Winga Cristiano Ronaldo amesema kwamba baada ya kustaafu soka ataufanyia kazi mpango wa kumiliki klabu ya soka.
Ronaldo kwa sasa ana mkataba na klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia ambao unafikia ukomo Juni 2025 lakini kwa sasa ameanza kupanga mambo yake ya baadaye nje ya soka la ushindani.
“Siwezi kujitoa katika wazo la kuwa mmiliki wa klabu,” alisema Ronaldo mbele ya waandishi wa habari jijini Madrid katika mkutano wa uzinduzi wa biashara yake mpya ya maji ya chupa.
“Ni jambo ambalo nililifikiria miaka michache iliyopita, ningependa niwe mmiliki wa klabu, naelekea mwisho wa maisha yangu ya soka katika miaka miwili au mitatu ijayo,” alisema.
Ronaldo, 38, ambaye alijiunga na Al Nassr Januari mwaka huu baada ya kuachana na Man United, pia alielezea kufurahishwa kwake na uamuzi wa nyota mwenzake wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema kuhamia Saudi Arabia.
Benzema, 35, alikataa kuongeza mkataba wa mwaka mmoja Real Madrid na badala yake akaamua kujiunga na klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia.
“Nilijua baada ya mimi kwenda Saudi Arabia nitakuwa nimefungua njia, Karim (Benzema) amekwenda na nina hakika wengine wengi watafuata, miaka miwili au mitatu Ligi ya Saudi itakuwa moja ya ligi muhimu duniani, ningependa wachezaji mastaa waje Saudi Arabia hakuna tatizo kwenye ligi, tunachotaka ni ushindani,” alisema Ronaldo.
Mchezaji mwingine aliyetarajiwa kwenda Saudi Arabia kujiunga na klabu ya Al-Hilal ni Lionel Messi aliyekuwa PSG ya Ufaransa lakini jana Jumatano ilithibitishwa kwamba ameamua kwenda nchini Marekani kujiunga na Inter Miami FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Mareakni.
Wachezaji wengine mastaa wanaotajwa kuwa na mipango ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia ni Sergio Busquets, N’Golo Kante, Jordi Alba, Roberto Firmino, Sergio Ramos, Angel Di Maria na Iago Aspas.