Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya Taifa ya England, Jude Bellingham kwa ada ya Pauni 88.5 milioni.
Bellingham kiungo ambaye ndio kwanza ana miaka 19, alisajiliwa Dortmund Julai 2020 akitokea klabu ya Birmingham City, kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na klabu za Real Madrid na Man City.
Man City na Real Madrid zilianza mbio za kumtaka kiungo huyo mara baada ya fainali za Kombe la Dunia, Desemba mwaka jana ambapo alikuwa mmoja wa wachezaji waliotamba katika fainali hizo zilizofanyika Qatar.
Habari zaidi zinadai kwamba kiungo huyo atasaini mkataba wa miaka sita na vigogo hao wa Hispania ambao hivi karibuni waliachana na mshambuliaji wao tishio, Karim Benzema aliyetimkia Saudi Arabia.
Ukiacha, Man City na Real Madrid, klabu nyingine iliyokuwa ikimtaka, Bellingham ni Liverpool lakini ilionekana kujitoa Februari mwaka huu kutokana na gharama zilizokuwa zikitajwa na kwa usajili huo huenda Bellingham akawa mchezaji ghali wa tatu kijana.
Bellingham ambaye pia ni nyota wa msimu katika Ligi Kuu Ujerumani yaani Bundesliga, pia huenda akawa mchezaji ghali zaidi wa pili wa England na mchezaji ghali zaidi wa pili wa Real Madrid baada ya Eden Hazard aliyejiunga na timu hiyo akitokea Chelsea mwaka 2019 kwa ada ya Euro 115 milioni.
Kimataifa Bellingham, Real Madrid kimeeleweka
Bellingham, Real Madrid kimeeleweka
Read also