Na mwandishi wetu
Yanga imetoka sare ya mabao 3-3 na Mbeya City wakati Simba ikiilaza Polisi Tanzania 6-1, Saido Ntibanzokiza akifunga mabao matano kati ya sita ya Simba na kufikisha mabao 15 katika Ligi Kuu NBC akimtikisa Fiston Mayele anayeshika usukani akiwa na mabao 16.
Katika mechi hizo za ligi hiyo zilizopigwa Jumanne hii, matokeo hayo yameibua gumzo jipya la nani ataibuka mfungaji bora msimu huu wa 2022-23? Je Ntibazonkiza (pichani juu) atambwaga Mayele?
Katika mechi za kukamilisha ligi hiyo zitakazopigwa Juni 9, Simba itakuwa mwenyeji wa Coastal Union wakati Yanga itakuwa mgeni wa Tanzania Prisons, mechi ambazo matokeo ya pointi yanaweza yasiwe na maana badala yake mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora zikateka hisia za mashabiki.
Kati ya mabao 15 aliyofikisha Ntibazonkiza hadi sasa, mengine aliyafunga wakati akiichezea Geita Gold wakati kwa Mayele yote ameyafunga akiwa na Yanga.

Kwa Mayele (pichani) iwapo ataangushwa na Ntibazonkiza, itakuwa mara ya pili mfululizo kukutana na hali inayofanana na hiyo, msimu uliopita alishindwa kutamba mbele ya George Mpole. Mayele alipigwa bao na Mpole katika mechi za mwisho na safari hii huenda akakutana tena na hali hiyo.
Zaidi ya hilo, Mayele atakuwa ameshindwa kutimiza ndoto yake aliponukuliwa akisema angependa kumaliza msimu huu akiwa mfungaji mwenye mabao mengi katika Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu NBC.
Tayari amefanikisha hilo kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kuongoza na mabao yake saba lakini kwenye Ligi Kuu NBC ametikiswa kidogo, Ntibazonkiza amemsogelea na haitoshangaza wakifungana kwa mabao au hata akapitwa.
Katika mechi ya Simba ukiacha mabao ya Ntibazonkiza, bao jingine la Simba lilifungwa na Israel Mwenda wakati bao pekee la Polisi likifungwa na Steven Mayala.
Yanga nao ambao tayari ni vinara wa Ligi Kuu NBC, matokeo ya mechi hiyo japo yamewaumiza mashabiki wake lakini yamezidi kuiweka pagumu Mbeya City ambayo ilitakiwa ishinde ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuepuka janga la kushuka daraja.
Wakati Polisi ikiwa tayari imeshuka daraja, Mbeya City yenye pointi 31 italazimika kupambana kufa na kupona ili ishinde mechi yake ya mwisho na KMC na hivyo kufikisha pointi 34.
Ugumu wa mechi hiyo unachangiwa na mazingira ya KMC yenye pointi 29 ambayo pia inahitaji ushindi ili ifikishe pointi 32. Je nani atashinda na kujinasua na janga la kushuka daraja? KMC kwa sasa inashika nafasi ya 14 wakati Mbeya City inashika nafasi ya 13.