Na mwandishi wetu
Koha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amesema wachezaji wake wanastaili pongezi kwa ushindi wa mabao 6-1 walioupata dhidi ya Polisi Tanzania kwani wameendelea kulinda heshima ya timu yao.
Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi huo mnono huku Saido Ntibazonkiza akifunga mabao matano ya Simba ingawa matokeo hayo pia yameishusha rasmi Polisi Tanzania katika Ligi Kuu NBC.
“Nawapongeza wachezaji wangu, wamecheza kwa kupigania heshima ya timu yao ingawa hakuna tunachopata baada ya kukosa ubingwa lakini imepunguza machungu kwa mashabiki wetu,” alisema Mgunda.
Kocha Msaidizi wa Polisi, John Tamba alikubaliana na matokeo hayo na kueleza kuwa wanarudi kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi ya Championship.
“Tulijitahidi kupambana lakini mambo yamekuwa tofauti, ni kweli tulizidiwa na tumekubali kilichotokea na sasa tunakwenda kujipanga ili kufanya vizuri kwenye Ligi ya Championship msimu ujao,” alisema Tamba.
Jana pia kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, mabingwa wa ligi hiyo, Yanga walilazimishwa sare ya mabao 3-3 na wenyeji Mbeya City ambapo Yanga wakilazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao matatu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema mechi hiyo ilikuwa mgumu kwao kutokana na uchovu waliokuwa nao wachezaji lakini anafurahi kuona wamepata pointi moja.
“Hatukuwa bora kwenye kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili mabadiliko tuliyoyafanya yametulipa, tumepata pointi moja ni kitu kizuri kwetu tunakwenda kujipanga kwa mchezo wetu wa mwisho ambao naamini tutakuwa bora ziaidi,” alisema Kaze.
Abdallah Mubiru ambaye ni kocha wa Mbeya City, alitupa lawama zake kwa mwamuzi wa mchezo huo, Tatu Malogo kutoka Tanga kwa madai alikuwa akiwapendelea wapinzani wao Yanga.
“Mwamuzi alionesha wazi kuipendelea Yanga kwa kuwavuruga wachezaji wangu, ukweli sijafurahishwa na hili ingawa nakubali kwamba Yanga ni timu nzuri lakini tuliwashika,” alisema Mubiru.
Soka Mgunda ataka Simba ipongezwe
Mgunda ataka Simba ipongezwe
Read also