Na mwandishi wetu
Bondia Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ anatarajia kupanda ulingoni Julai 15, mwaka huu kuzichapa na Erick Katompa katika pambano la raundi 10 linalotarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Sabasaba, Dar es Salaam.
Pambano hilo litakuwa la marudiano baada ya lile la awali lililofanyika Oktoba 10, 2021 na Mbabe kupigwa kwa pointi na mpinzani wake huyo.
Muandaaji na promota wa ngumi za kulipwa nchini, Meja Selemani Semunyu alisema tayari wamekamilisha kila kitu ikiwemo mabondia kusaini mikataba na kwa sasa Dulla Mbabe yupo katika maandalizi mazito kumkabili Katompa.
“Tuna imani kubwa na Dulla sababu ni bondia mkubwa nchini na tunajua uwezo wake ingawa hapa kati alipitia changamoto za hapa na pale lakini kuelekea pambano hilo tumemwandaa vizuri ikiwemo kuweka kambi kwa Kocha Master Kinyogoli ambaye anasifika kwa ngumi za mahesabu nchini,” alisema Semunyu.
Semunyu alisema kuwa Dulla Mbabe anahitaji kuendelea kuleta ladha ya mchezo huo kwa kuwa mabondia wengine wanamtumia kama mfano na sababu ya wao kuingia kwenye mchezo wa masumbwi nchini na ni kivutio kwa wadau na wadhamini pia.
Semunyu alisema pambano hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora waliokuwa nao mabondia wote wawili ingawa Dulla analazimika kushinda pambano hilo ili kurudisha imani kwa mashabiki wake ambao kwa kiasi fulani wamekuwa wanyonge baada ya kupoteza pambano la kwanza.
Ngumi Dulla Mbabe ulingoni Julai 15
Dulla Mbabe ulingoni Julai 15
Read also