Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Senegal kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Afcon 2023 dhidi ya Benin.
Sakho (pichani) ameitwa kwenye kikosi hicho na kocha mkuu wa timu hiyo, Aliou Cisse kwa mara ya pili baada ya awali kuitwa Machi mwaka huu walipokuwa wakijiandaa kuuamana na timu ya taifa ya Msumbiji.
Senegal iliyoita jumla ya wachezaji 26 itavaana na Benin ikiwa ugenini Juni 17 mjini Cotonou kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Brazil Juni 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa José Alvalade mjini Lisbon, Ureno.
Cisse hata hivyo amewatema mshambuliaji wa Lorient, Bamba Dieng na kipa wa Chelsea, Edouard Mendy katika kikosi hicho na kuwajumuisha winga Ismail Jacobs wa AS Monaco, kiungo Pape Gueye (Sevilla) na Cheikhou Kouyate (Nottingham Forest) aliyerejea kikosini baada ya awali kukosekana kutokana na majeraha.
Baadhi ya nyota wengine walioitwa kwenye kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Afcon ni Sadio Mane wa Bayern Munich, Kalidou Koulibaly (Chelsea), Gana Gueye (Everton), Ismaila Sarr (Watford) na Abdou Diallo (RB Leipzig).
Senegal inaongoza Kundi L ikiwa na pointi 10, ikifuatiwa na Msumbiji yenye pointi nne, Rwanda ya tatu ikiwa na pointi tatu huku Benin ikiburuza mkia kwa pointi mbili baada ya timu zote kucheza mechi nne.
Kimataifa Pape Sakho aitwa timu ya Taifa
Pape Sakho aitwa timu ya Taifa
Read also