Na Hassan Kingu
Yanga kesho Jumamosi itashuka dimbani kwenye fainali ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger. Fainali ya kwanza, Yanga ikiwa nyumbani ililala kwa mabao 2-1.
Kesho Yanga itakuwa na kibarua kingine Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers ikitaka kujiuliza juu ya matokeo ya awali lakini pia kuhakikisha haipotezi ubingwa wa Shirikisho uliobakiza dakika 90 pekee kumtambua bingwa mpya.
Mpira unadunda, hauna mwenyewe, haupaswi kukosewa heshima; hizi ni kauli za kibabe za soka katika kujipa matumaini ya kupindua meza, kauli ambazo bila shaka Yanga inatembea nazo.
Lakini baada ya kauli hizo tukirejea kwenye hali halisi, Yanga ina kazi ya kufanya kupindua meza ugenini na kutawazwa mabingwa wapya na kuweka rekodi mpya kabisa Ukanda wa Cecafa (Baraza la Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati).
Yanga ikifanya hivyo itakuwa timu ya kwanza Cecafa kupindua meza ugenini katika fainali hizo na kunyakua ubingwa. Kombe hili halijawahi kwenda Cecafa na Cosafa (Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika) pekee.
Wanajangwani hao wamekuwa wakipindua meza na kuruka viunzi kadhaa tangu kuanza kwa michuano hii msimu huu. Nachelea kusema Yanga wanayaweza haya mapambano bila ya kushusha hadhi ya mchezo ulio mbele yao.
Yanga ilianza kuweka alama zake ikitinga hatua ya makundi baada ya kuibonda Club Africain ya Tunisia kwa bao 1-0 ugenini baada ya mechi iliyopigwa kwa Mkapa kuisha kwa suluhu.
Haikuishia hapo, kwenye mechi sita za hatua ya makundi, Yanga imepoteza moja ugenini dhidi ya US Monastir kabla ya ushindi wa mechi nne na sare moja bila ya kupoteza uwanja wa nyumbani.
Ilipofika robo fainali iliibugiza Rivers United ya Nigeria iliyokuwa kwao mabao 2-0 kabla ya suluhu Yanga ilipokuwa nyumbani na hivyo kupenya nusu fainali kwa ushindi wa ugenini.
Nusu fainali ilipokutana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini, waliichapa mabao 2-0 kwa Mkapa kabla ya kuichapa tena mabao 2-1 kwao na kuvunja mwiko wa timu hiyo kutofungwa nyumbani katika kombe hilo msimu huu.
Kwa mantiki hiyo, mpaka Yanga inafika fainali imekuwa ikinufaika na mechi za ugenini lakini je, kesho itafanikiwa kutembea na mwendo huo mbele ya kocha Abdelhak Benchikha aliyeipa RS Berkane ndoo ya Super Cup msimu huu kwa kuifunga Wydad CA mabao 2-0? Ni suala la kusubiri.
Hata hivyo, USMA inaitolea macho fainali hii ikitaka kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza ikiwa ndio mara ya kwanza pia kuingia fainali ya michuano hiyo, kama vile ambavyo Yanga imeingia kwa mara ya kwanza.
USMA imepania kuweka rekodi ya kuchukua ndoo hiyo kwani hii ni mara ya pili inacheza fainali ya michuano ya klabu Afrika, awali iliingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na kupoteza kwa jumla ya mabao 4-1 mbele ya TP Mazembe, Mbwana Samatta akifunga mabao mawili.
Na Waalgeria hao wanaamini hii ni nafasi kwao kwa kuwa wamebakiza mechi moja nyumbani na hawajapoteza mchezo wowote kwao msimu huu katika michuano hiyo.
Kwanza ilitinga hatua ya makundi kwa ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 dhidi ya Cape Town City baada ya suluhu ya mechi ya nyumbani.
Kwenye makundi, USMA ilishinda mechi tatu nyumbani, sare mbili na kufungwa mechi moja ugenini na Gallants. Kwenye robo fainali ikaipasua AS FAR kwa mabao 2-0 nyumbani kabla ya kukubali kichapo cha mabao 3-2 ugenini.
Nusu fainali ikaikazia Asec Mimosas na kutoka suluhu ugenini na walipokwenda Algeria ikaibomoa Asec mabao 2-0.
Kwa kifupi, USMA haijafungwa kwake kama ilivyokuwa Yanga msimu huu mpaka pale ilipoharibiwa rekodi hiyo na USMA wenyewe Mei 28, mwaka huu na sasa utagundua Yanga haichezi mechi ya leo kwa kuwania kombe pekee bali kutibua pia rekodi ya wababe hao wa Kaskazini ya kutofungwa kwao.
Yanga hata hivyo itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya kuwa na mfungaji bora wa michuano hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Fiston Mayele amefunga mabao saba mpaka sasa akiwa amefunga kwenye kila hatua ambapo mabao matatu amefunga hatua ya makundi, mawili robo fainali, moja nusu fainali na jingine kwenye mchezo wa kwanza wa fainali.
Ranga Chivaviro wa Gallants mwenye mabao sita, Paul Acquah (Rivers), Aubin Kouame (Asec) wenye mabao manne kila mmoja, timu zao zimetoka na nafasi ya kupambana na Mayele angalau inaonekana kwa Khaled Bousseliou wa USMA mwenye manne pia.
Ingawa lolote linaweza kutokea na kuandikwa rekodi mpya ya mfungaji bora wa Shirikisho aliyefunga ‘hat-trick’ kwenye fainali ya mwisho lakini hilo halizuii ukweli kuwa ni jambo gumu kulishuhudia.
Yote kwa yote, mechi ya kesho ni mechi ya rekodi kuanzia kwa Yanga kupindua meza na kushinda ugenini fainali, kutoa mfungaji bora na kuwa timu ya kwanza Cecafa kufanya hivyo.
Kwa USMA pia nayo inatazamia kuyafanya hayo kwa upande wao na kuchukua kombe la kwanza la klabu baani Afrika.