Manchester, England
Straika wa Man City, Erling Haaland amesema atafanya kila liwezekanalo ili kuiwezesha timu yake kuweka historia kwa kubeba mataji matatu au ‘treble’ msimu huu wa 2022-23.
Man City tayari imebeba taji la Ligi Kuu England (EPL) na inaweza kubeba taji la pili kesho Jumamosi ikiifunga Man United katika fainali ya Kombe la FA na Juni 10 itaivaa Inter Milan katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man Unted ndio timu pekee na ya mwisho katika EPL kuwahi kubeba mataji matatu katika msimu mmoja, ilifanya hivyo mwaka 1999 wakati huo ikinolewa na Sir Alex Ferguson.
“Itakuwa si jambo la uhakika kutoweka hii historia,” alisema Haaland mwenye umri wa miaka 22 na ambaye ndiye kinara wa mabao EPL msimu huu akiwa na mabao 36.
“Hii ndio sababu hasa ya wao kuninunua mimi, ni ili tufike hatua hii, hatuna sababu ya kulificha jambo hilo, itakuwa na maana kubwa na nitafanya kila liwezekanalo kujaribu kufanikisha hili, ni ndoto yangu kubwa na ni matumaini yangu ndogo hii itakuwa kweli,” alisema Haaland.
“Lakini pia nafahamu kwamba si jambo rahisi, ni fainali ya timu mbili nzuri ambazo kila moja itafanya kila linalowezekana kujaribu kumuharibia mwenzake,” aliongeza Haaland.
“Tumekuwa tukilipigania hili kwa msimu mzima, tuliposhinda taji la ligi kuu ilikuwa faraja kubwa, na sasa tuna fainali mbili zimebaki na kitu pekee tunachoweza kukiangalia kwa sasa ni fainali hizo kabla ya kwenda mapumziko,” alisema Haaland.
Man City ikiwa chini ya kocha Pep Guardiola imekuwa ikitamba England katika miaka ya karibuni lakini haijawahi kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu huu timu hiyo inapewa nafasi kubwa ya kubeba taji hilo kubwa na lenye hadhi kwa michuano ya ngazi ya klabu barani Ulaya na duniani kwa ujumla.