Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino (pichani) ameipongeza klabu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2022-23.
Pongezi hizo zilizotumwa kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia zimeisifu Yanga kwa bidii ya timu iliyokuwa nayo, ari na kujitolea kwa msimu mzima ndizo zilizopelekea vijana hao wa Jangwani kutwaa ubingwa huo.
“Isingekuwa rahisi kutwaa ubingwa huo bila ya bidii ya timu nzima, ari na kujitolea, kila mtu kwenye klabu anaweza kujivunia hilo na ni pongezi kwa kila mmoja wa wote waliohusika katika mafanikio hayo,” ilieleza sehemu ya ujumbe wa Infantino kupitia taarifa iliyowekwa na TFF kwenye vyanzo vyake vya habari.
Katika pongezi zake hizo pia Infantino ameipongeza TFF kwa mchango wake katika mandeleo na ustawi wa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Yanga imefanikiwa kutetea taji lake hilo wiki mbili zilizopita kwa kuifunga Dodoma Jiji mabao 4-2 na kufikisha pointi 74 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine 15 zilizobaki katika msimamo wa ligi hiyo maarufu kwa sasa Afrika.
Timu hiyo inatwaa taji hilo kwa msimu wa pili mfululizo baada ya awali kulikosa kwa misimu minne mfululizo walipokuwa wakilishuhudia likitua kwa mahasimu wao, Simba SC.
Kimataifa Rais Fifa aipongeza Yanga
Rais Fifa aipongeza Yanga
Read also