Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Geita Gold umeeleza kuwa upo kwenye mchakato wa kuandaa tuzo za msimu kwa ajili ya wachezaji wa timu hiyo kuanzia msimu ujao wa 2023-24.
Ofisa Habari wa Geita, Samwel Dida ameiambia GreenSports leo Jumanne kuwa kwa sasa wapo kwenye majadiliano ya kina kuhakikisha wanalitekeleza kwa weledi mkubwa jambo hilo kwa ajili ya kuthamini mchango wa timu nzima kwa kila mchezaji.
Alisema tuzo hizo zitakuwa ni kwa ajili ya mchezaji bora wa kila mwezi katika miezi minane ya msimu mzima, mchezaji bora wa kila mechi na tuzo za idara mbalimbali ndani ya uwanja mwisho wa msimu.
“Timu imekuwa ikipambana mno, msimu uliopita tulimaliza kwenye nne bora na msimu huu tunapambana kumaliza tano bora. Kwa hiyo ni mwenendo mzuri na katika kulithamini hilo tupo kwenye mchakato wa kuwaandalia tuzo, tunahitaji wapate stahiki yao mwisho wa mapambano,” alisema Dida.
Geita iliyopanda kushiriki ligi kuu msimu wa 2021-22, msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza. Msimu huu zimesalia mechi mbili kumalizika kwa ligi, ikiwania kumaliza juu ya Namungo iliyo nafasi ya tano kwa pointi 39 wakati Geita ina pointi 37.