Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo, Sébastien Desabre ameita kikosi chake akiwajumuisha Fiston Mayele wa Yanga na Henock Inonga wa Simba kwa ajili ya kuivaa Gabon katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2023.
Mayele anaitwa kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kiwango anachoendelea kukionesha kwenye michuano inayoshiriki Yanga ikiwemo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako mchezaji huyo anaongoza kwa mabao saba.
Na licha ya Simba kushindwa kutwaa taji lolote msimu huu lakini kiwango cha Inonga kimeendelea kung’ara na kumshawishi Desbare kumwita kwenye kikosi hicho chenye wachezaji 27.
Kabla ya kuivaa Gabon Juni 18, DR Congo itacheza na Uganda mechi ya kirafiki itakayopigwa Juni 14, mwaka huu mjini Douala, Cameroon.
Congo inahitaji ushindi dhidi ya Gabon ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya Kundi I ambako inaburuza mkia kwa pointi nne baada ya mechi nne ikiwa imeshinda mchezo mmoja, sare moja na kufungwa mara mbili.
Pia, Congo ikiwa ugenini Uwanja wa Franceville, mjini Franceville itahitaji ushindi kulipa kisasi kwa Gabon iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi iliyopita iliyopigwa Uwanja wa Martyrs, Kinshasa, DR Congo.
Mara ya mwisho, Chui hao kushiriki michuano ya Afcon ilikuwa mwaka 2019 walipopangwa kundi moja na Misri, Zimbabwe na Uganda ambapo Desabre ndiye aliyekuwa kocha wao wakati huo.