Na mwandishi wetu
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Mwanamtwa Kihwelo ameieleza Yanga kulingana na ujanja wa timu ya USM Alger ya Algeria wanayokutana nayo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ni vyema wakapata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya awali.
Kihwelo ameeleza hayo akifafanua kuwa USMA ni timu nzuri ndio maana imefika fainali na kutokana na hatua ya mchezo wenyewe ni vizuri Yanga ikategemea zaidi matokeo ya nyumbani safari hii kuliko ugenini.
“Tunapaswa kujipanga vizuri sababu mpinzani pia sio mbaya, anafahamika na amefika fainali kwa kupambana, kikosi cha Yanga nakiaminia na nakitegemea lakini lazima ipambane kupata ushindi nyumbani,” alisema mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Simba.
“Zimesalia mechi mbili tu hivyo ni bora kuchanga karata mapema nyumbani, mfano tukiwafunga mabao mawili au matatu, kisha tukiwa ugenini tucheze kwa akili wakati wao watataka kufunguka na ndipo Yanga itakapotumia vizuri zile ‘counter attack’ na kufunga,” alisema Kihwelu nyota wa zamani wa Taifa Stars.
Kihwelo ameeleza kwamba hana wasiwasi na mwendo iliokuwa nao Yanga mpaka kufika fainali kwa matokeo ya mechi zao za ugenini lakini ni vyema wakatafuta uhakika wakiwa uwanja wa nyumbani.
Yanga ambayo iliifunga Rivers United ya Nigeria mabao 2-0 kwao kisha kwenye nusu fainali kuibomoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini nyumbani na ugenini, itaanzia fainali ya kwanza Mei 28 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Fainali ya pili itachezwa Juni 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers.