Na mwandishi wetu
Hatimaye imesalia siku moja kabla ya kupigwa mechi ya fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na USM Alger ya Algeria huku makocha wa timu zote wakitamba kutaka ushindi kwenye mechi hiyo.
Akizungumza leo Jumamosi, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema fainali hiyo itakuwa na ufundi mkubwa kutokana na mipango waliyonayo na ya wapinzani wao ambao watahitaji matokeo kama wao katika mechi hiyo.
Nabi aAlisema anawafahamu Waalgeria juu ya jihad ya kujitolea waliyonayo lakini hata Yanga wataingia na nguvu ya tofauti katika mchezo huo wakifahamu wanaipambania bendera ya Tanzania katika fainali hiyo ya kwanza kihistoria ya michuano hiyo.
“Tunacheza na timu kubwa ndio maana wapo fainali, haitakuwa rahisi kama mashabiki pengine wanavyotaka sababu tuko nyumbani tufunge mabao mengi, wachezaji wakiingia kwenye huo mtego, mechi imeharibika.
“Nimefundisha jirani na Algeria, tunafahamiana na sisi Watunisia, wote wana ‘tabia za Italia’ za kujitolea, kujituma wakijua wanataka kupata kitu, hata sisi Yanga tuna ‘tabia yetu ya kujitolea’, kujituma kuangalia kwana bendera ya Tanzania, kwahiyo najua wachezaji wote wako tayario na hilo,” alisema Nabi.
Nabi pia, alieleza kusikitishwa kwa kumkosa kiungo, Khalid Aucho katika mechi hizo mbili za fainali kutokana na kuwa na kadi za njano sita lakini anaamini uwepo wa wachezaji wengine kwenye nafasi yake watafanya vizuri kutokana na uwezo mkubwa walionao.
Kocha Mkuu wa USMA, Abdelhak Benchikha alisema anaamini mechi iko nusu kwa nusu kutokana na ubora wa timu zote ingawa hata kama yuko ugenini hatoruhusu kukaba tu bali watacheza soka kwa kushambulia kama wako kwao Algeria.
“Mimi na vijana wangu tunawaza kujitahidi kuzuia njia za wapinzani, tutahitaji kumiliki mpira na kushambulia, hatutakaa nyuma kama wacheza tenisi, sisi ni timu ya mpira, hatutacheza kama tupo ugenini, tutacheza kama tuko nyumbani, ndiyo maana ya mpira,” alisema Benchikha.
Kocha huyo alieleza kutambua uwepo wa mshambuliaji Fiston Mayele wa Yanga lakini akasema hamuhofii huyo pekee kwani Yanga ina wachezaji wengi hatari na wenye kasi kama Tuisila Kisinda aliyewahi kumfundisha akiwa RS Berkane ya Morocco, hivyo anafahamu mchezo hautakuwa mwepesi.
Baada ya mchezo huo utakaopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, timu hizo zitarudiana kwenye fainali ya pili itakayopigwa Juni 3, mwaka huu Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers.
Timu hizo ambazo zote zinacheza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza, zimeingia fainali baada ya Yanga kuibutua Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1 wakati USMA iliichapa Asec Mimosas ya Ivory Coast mabao 2-0.
Kimataifa Makocha Yanga, USMA wataka ushindi
Makocha Yanga, USMA wataka ushindi
Read also