Munich, Ujerumani
Dakika chache baada ya Bayern Munich kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga leo Jumamosi ikiwa ni mara ya 11 mfululizo, klabu hiyo imemfuta kazi Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO). Oliver Kahn.
Sambamba na Kahn ambaye ni kipa wa zamani wa Bayern aliyejipatia umaarufu na timu hiyo, kiongozi mwingine aliyefutwa kazi hapo hapo ni mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Hasan Salihamidzic.
Kahn (pichani) aliteuliwa kuwa CEO wa Bayern mwaka 2021 akichukua nafasi ya Karl-Heinz Rummenigge na baada tu ya kutimuliwa hii leo, Jan-Christian Dreesen alitangazwa hapo hapo kuwa CEO mpya. Ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
“Ulikuwa uamuzi mgumu wa kuachana na Oliver lakini tulifikia hitimisho hilo kwa kuzingatia mpango mzima wa maendeleo na kufanya mabadiliko ya nafasi za maofisa kwenye bodi,” ilifafanua taarifa hiyo.
Bayern leo imecheza na FC Cologne na kuichapa mabao 2-1 ikiokolewa na bao la dakika ya 89 mfungaji akiwa Jamal Musiala lakini pia matokeo ya sare ya mabao 2-2 iliyoyapata Borussia Dortmund ndiyo yaliyoifanya Bayern ibebe taji kwa tofauti ya mabao.
Msimu huu haukuwa mzuri kwa Bayern ambayo imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Ujerumani na Ligi ya Mabingwa Ulaya, yote katika hatua ya robo fainali licha ya kumtimua kocha Julian Nagelsmann na nafasi yake kuchukuliwa na Thomas Tuchel.
Akizungumzia kutimuliwa kwake Kahn alitumia mtandao wa Twitter kuipongeza timu na baada ya hapo akasema, “nilipenda kusherehekea ubingwa na wachezaji lakini bahati mbaya sijaweza, siwezi kuwa nao leo kwa sababu sikuruhusiwa.”
“Haukuwa msimu ambao tunaweza kuufurahia, haukuwa msimu ambao idadi ya pointi zimetosha kwa mahitaji yetu, ni msimu ambao kiwango cha uchezaji wetu kilitutosha sisi tu, vyovyote ilivyokuwa mwisho wa siku haukuwa msimu wa kuridhisha hata kidogo,” alisema Kahn.