London, England
Straika wa Liverpool, Mohamed Salah (pichani) ameshtushwa kwa kitendo cha timu hiyo kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao na kuongeza kuwa hakuna msamaha kwa hilo.
Salah alitoa kauli hiyo kwenye mitandao ya kijamii baada ya timu hiyo kushindwa kumaliza ‘top four’ kwenye Ligi Kuu England (EPL) na sasa timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tano itacheza Europa Ligi msimu ujao.
“Tumewaangusha nyinyi mashabiki na tumejiangusha sisi wenyewe,” alisema Salah ambaye msimu uliopita alikuwa kinara wa mabao EPL.
Timu zilizofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ni vinara wa EPL, Man City, Arsenal walioshika nafasi ya pili, Man United walioshika nafasi ya tatu na Newcastle wanaokamilisha top four.
“Tulikuwa na kila kitu tulichohitaji ili kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao lakini tumeshindwa,” alisema Salah ambaye pia alikuwa na kikosi hicho kilichobeba taji la ligi hiyo kubwa na yenye hadhi msimu wa 2018-19 lakini iliishia fainali msimu uliopita na kushindwa kutamba mbele ya Real Madrid.
Liverpool ilianza kampeni zake EPL msimu huu kibabe ikitoka na ushindi mbele ya Man City katika mechi ya Ngao ya Jamii lakini baada ya hapo walishinda mechi mbili tu kati ya nane za mwanzo za EPL.
Kwa upande wa Salah ambaye msimu uliopita alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu na Liverpool, msimu huu ameifungia timu hiyo mabao 19.