Roma, Italia
Kocha wa AS Roma ya Italia, Jose Mourinho amesema kwamba Tottenham Hotspur ni klabu pekee ambayo amewahi kuwa kocha wake lakini hana mawasiliano nayo baada ya kuondoka kwake.
Mourinho ambaye pia amewahi kuzinoa klabu za Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na FC Porto, alitimuliwa Spurs Aprili 2021 ikiwa ni miezi 17 baada ya kupewa kibarua cha kuinoa timu hiyo.
“Ni matumaini yangu kwamba mashabiki wa Tottenham hawatanichukulia vibaya lakini klabu pekee katika maisha yangu ya kuwa kocha ambayo nimeendelea kutovutiwa nayo ni Tottenham,” alisema Mourinho.
“Labda kwa sababu uwanja ulikuwa hauna mashabiki kipindi cha korona, labda kwa sababu Bwana Levy (mwenyekiti wa Tottenham Daniel Levy) hakunipa nafasi ya mwisho ya kushinda kombe.”
Kauli za Mourinho zimekuja siku chache baada ya jana Alhamisi, kocha wa Feyenoord ya Uholanzi, Arne Slot kukataa kibarua cha kuinoa Spurs.
Mourinho aliulizwa kuhusu mambo yake ya baadaye na Roma ambapo alisema ataendelea kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na klabu hiyo kama ilivyo kwa klabu nyingine alizowahi kuzifundisha.
“Tutaendelea kuwa na mawasiliano kwa wakati wote, ni kama ilivyo kwa klabu zangu nyingine za hapo kabla, ukiacha klabu ya Bwana Levy,” alisema Mourinho.
“Hiyo ndiyo klabu pekee, ukiacha hiyo (Spurs) nyingine za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Manchester United, Real Madrid, klabu zote hizo najiona niko pamoja nazo, watu wanaweza kusema huwezi kupenda klabu zote, ndio mimi nazipenda klabu zote hizo,” aliongeza Mourinho.
Mourinho alitimuliwa Spurs wiki moja kabla ya timu hiyo kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Man United, mechi ambayo Spurs ililala kwa bao 1-0 wakati huo ikinolewa na kocha wa muda, Ryan Mason.
Baada ya kutimuliwa Spurs, Mourinho aliibukia AS Roma ambayo msimu uliopita aliiwezesha kubeba taji la michuano mipya ya klabu barani Ulaya ya Europa Conference Ligi na kwa sasa Roma inasubiri kuumana na Sevilla katika mechi ya fainali ya Europa Ligi itakayopigwa Mei 31.
Mambo yakienda vizuri, Mourinho anaweza kutangaza taji lake la pili la Ulaya na klabu hiyo. Hadi sasa ana rekodi ya mataji matano Ulaya, mawili ya Ligi ya Mabingwa, mawili ya Europa Ligi na moja la Europa Conference Ligi.