Na mwandishi wetu
Kiungo wa Simba, Cletous Chama amesema amekuwa akitumiwa jumbe mbalimbali za kumkosoa kutoka kwa mashabiki baada ya timu yao kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa msimu huu.
Nyota huyo alisema hayo yote ni kwasababu wameteleza msimu huu kwa kushindwa kuwapa mashabiki zao furaha iliyostahili.
Alisema mashabiki wamekuwa pamoja nao na kuna wakati wanawatia moyo na kuwasapoti na wakati mwingine amekuwa akipata ujumbe wa kumpinga na kumkosoa, akikiri kwamba maisha ndivyo yalivyo wakati mwingine.
“Nawashukuru mashabiki msimu huu wamekuwa na sisi, kuna muda wanalalamika ndio maana kama hawajapenda lazima waongee. Kwangu tunathamini mchango wao kwenye timu na maisha yetu, tumeteleza kidogo lakini ndivyo maisha yalivyo,” alisema Chama.
Chama alisema mashabiki wamekuwa wakitaka kuona mambo makubwa kutoka kwake ndio maana changamoto za kukosolewa zimekuwa zikitokea pale ambapo wanashindwa kuona walichotarajia.
“Sisi kama wachezaji lazima tufanye tathmini kuona nini tumechangia kwenye msimu. Tuangalie vitu vibaya tulivyofanya tujirekebishe na vile vizuri tuendelee navyo kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao,” alisema Chama.
Huu ni msimu wa pili mfululizo miamba hiyo inashindwa kuondoka na kombe lolote baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC, kutolewa nusu fainali Kombe la FA (ASFC), pia wakiishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.