Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga umesema kuwa kiungo wao Feisal Salum ‘Fei Toto’ atakabidhiwa medali yake ya ushindi wa Ligi Kuu NBC na endapo itabeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, atapewa pia.
Mwanasheria wa klabu hiyo, Simon Patrick alisema wanatambua Fei Toto ni mchezaji wao halali hivyo ni haki yake kama wachezaji wengine kupata medali ya ubingwa wowote utakaochukuliwa na klabu.
“Medali yake ya ubingwa wa ligi kuu ipo na atapata, pia kama tukichukua Kombe la Shirikisho Afrika atapata medali yake pia,“ alisema Patrick.
Tayari Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC baada ya mechi 28 na kesho Jumapili wanatarajia kucheza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA (ASFC) huku pia wakiwa wamefuzu kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Fei hajaichezea Yanga tangu Desemba, mwaka jana baada ya kuomba kuvunja mkataba na klabu hiyo na kulipa gharama za mkataba wake.
Ombi la mchezaji huyo hata hivyo lilikataliwa na klabu hiyo hali iliyomfanya kuendelea kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu licha ya kukata rufaa TFF na kugonga mwamba zaidi ya mara mbili.
Mkataba wa mchezaji huyo wa zamani wa JKU ya Zanzibar unatarajiwa kufika tamati ifikapo Mei 30, mwakani.