Na mwandishi wetu
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra ameongoza kwa kuwania vipengele vitatu vya tuzo za TFF msimu wa 2022-23 vilivyotangazwa leo Jumamosi huku swali likibaki je atabeba tuzo zote hizo?
Kipa huyo anafuatiwa na mshambuliaji Fiston Mayele, kipa Benedict Haule, Clement Mzize (Yanga), Bruno Gomes (Singida Big Stars), Mzamiru Yassin na Saido Ntibazonkiza (Simba SC) wanaowania vipengele viwili kila mmoja.
Kwa mujibu wa kamati ya tuzo hizo, Diarra anayeongoza kwa ‘clean sheet’ 16 kwenye ligi mpaka sasa ameibuka kinara katika mgawanyiko wa makundi mawili ya tuzo hizo ambazo ni tuzo za ligi kuu na za Kombe la FA (ASFC).
Tuzo nyingine zilizotangazwa na kamati hiyo ni tuzo za Ligi Kuu Wanawake, tuzo za utawala na tuzo za ligi nyingine.
Diarra anawania tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu dhidi ya Mayele, Gomes, Mzamiru na Ntibazonkiza pia jina lake likipenya kwenye tuzo ya kipa bora wa ligi hiyo sambamba na Aishi Manula wa Simba na Haule.

Kipa huyo ambaye amekuwa na mwendelezo wa mafanikio kwa msimu wa pili sasa, kipengele kingine anachowania tuzo ni kile cha kipa bora wa Kombe la FA, akiwania dhidi ya Haule na Abdulai Iddrisu wa Azam.
Tuzo ya kiungo bora yumo Gomes, Mzamiru, Ntibazonkiza, Clatous Chama wa Simba na Stephane Aziz Ki wa Yanga wakati wanaowania tuzo ya beki bora ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto (wote Yanga), Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na Henock Inonga (wote Simba).
Tuzo ya kocha bora inawaniwa na Mtunisia, Nasreddine Nabi wa Yanga, Mbrazil, Roberto Oliveira wa Simba na kocha wa Singida BS, Hans van Der Pluijm raia wa Uholanzi.
Tuzo ya mchezaji bora chipukizi wamo Clement Mzize wa Yanga, Edmund John wa Geita Gold na Lameck Lawi (Coastal Union).
Mzize pia anawania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya U20 dhidi ya William Mwani wa Mbeya Kwanza na Ladaki Chasambi (Mtibwa Sugar).
Timu za Ruvu Shooting, KMC na Tanzania Prisons zimetajwa kuwania tuzo ya timu yenye nidhamu huku tuzo ya bao bora ligi kuu ikielezwa kuwa mabao shiriki yameshapatikana lakini zinasubiriwa kukamilika kwa mechi mbili zilizosalia kwa kila timu kupata orodha kamili.
“Lakini wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la FA, wateule watatangazwa kesho Jumapili baada ya mechi ya nusu fainali ya pili baina ya Singida BS na Yanga itakayopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.
Upande wa tuzo ya kipa bora wa Ligi ya Wanawake inawaniwa na Najiath Abbas wa JKT Queens, Winfrida Jedah wa Fountain Gate na Gelwa Yona wa Simba Queens. Chipukizi Bora yumo Winfrida Charles wa Alliance Girls dhidi ya Winfrida Gerald (Fountain) na Jackline Shija (JKT).
Mshambuliaji wa Simba, Jentrix Shikangwa (pichani chini) ambaye ni mfungaji bora wa ligi hiyo kwa mabao 17 yumo kwenye kipengele cha mchezaji bora dhidi ya Donisya Minja wa JKT na Amina Bilal wa Yanga Princess.

Nao makocha Ally Ally wa JKT, Juma Hussein wa Fountain Gate na Charles Lukula wa Simba wanawania tuzo ya kocha bora wakati kipengele cha timu yenye nidhamu kimewapambanisha Amani Queens, JKT Queens na Alliance Girls.