London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kwamba kikosi chake kimepiga hatua kubwa msimu huu bila ya kujali jinsi walivyocheza mechi zao mbili za hivi karibuni za Ligi Kuu England (EPL).
Arsenal hadi Desemba mwaka jana ilikuwa ikishikilia usukani wa EPL kwa tofauti ya pointi saba lakini sasa inashika nafasi ya pili ikiwa imezidiwa na Man City wanaoshika usukani kwa tofauti ya pointi nne.
Kesho Jumamosi timu hiyo itakuwa ugenini dhidi ya Nottingham Forest timu inayopambana kujinasua na janga la kushuka daraja lakini iwapo Arsenal itapoteza mechi hiyo, Man City itatangazwa kinara wa EPL msimu huu.
“Tumejenga msingi huo imara, kuna viwango bora, vijana wengi, utayari wa hali ya juu lakini pia tumezungukwa na watu wengi wazuri wenye uzoefu sahihi, viongozi wengi wapo karibu,” alisema Arteta.
“Tunatakiwa kuendelea na hilo kwa sababu ya uhitaji, matarajio na hata changamoto za msimu ujao zitakuwa juu zaidi,” alisema Arteta.
Mambo yalianza kuwaharibikia Arsenal mwezi uliopita baada ya kupata sare mfululizo dhidi ya Liverpool, West Ham na Southampton kabla ya kukubali kipigo cha mabao 4-1 mbele ya Man City.
Alipoulizwa kama uchezaji wa Arsenal msimu huu umewapa maumivu, Arteta alijibu, “inategemea maumivu hayo ni ya nini, kuna matukio mengi ya kuvutia na yanayoridhisha kwa jinsi tulivyocheza, ngoja tuone tutamalizaje mechi mbili zilizobaki.”
“Maumivu ni sehemu ya soka, usiposhinda, usipocheza katika kiwango chako inauma, ni lazima iume katika namna sahihi na unatakiwa kutumia maumivu hayo ili kuwa bora na kutafuta majibu na suluhisho la kukusaidia kushinda zaidi,” alifafanua Arteta.