Na mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa mara nyingine ameipongeza Yanga kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akisisitiza wameipa heshima nchi na kuahidi kununua kila bao Sh milioni 20.
Rais Samia alisema hayo baada ya Yanga kuitoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1 na sasa itacheza fainali na USM Alger ya Algeria.
“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Yanga kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mmeandika historia na kuipa nchi yetu heshima kubwa sana. Nawatakia kila la heri katika mchezo wenu wa fainali,” aliandika Rais Samia kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Rais Samia pia leo Alhamisi wakati akizindua minara ya mfumo wa urushaji matangazo ya televisheni ya Azam Media Limited kwa kutumia antena yaani mfumo wa Digital Terrestrial Television (DTT), alisema Serikali itatoa ndege kuipeleka Yanga Algeria na kila bao watakalofunga kwenye fainali atatoa Sh milioni 20.
“Nawapongeza Yanga kwa kufika fainali ila hata Simba japo imeishia njiani, timu hizi zilipoanza mashindano niliwapa motisha lakini kuanzia sasa kila bao litakalofungwa nitatoa Sh milioni 20 na Serikali itatoa ndege kwenda Algeria na itawasubiri hadi mechi imalizike,” alisema Rais Samia.
Rais Samia hata hivyo alifafanua kwamba bao litakalolipiwa fedha hizo ni lile ambalo litasababisha ushindi kwa timu na si vinginevyo.
Awali, Rais Samia alianza kwa kutoa Sh milioni 5 kwa kila bao kwenye hatua ya makundi ya michuano ya klabu Afrika kwa timu za Simba na Yanga kabla ya kupanda hadi Sh milioni 10 kwenye mechi za nusu fainali. Kwenye motisha hiyo hadi sasa Yanga imechota Sh milioni 100.
Pia aliwataka viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha wanaisaidia na kuipa moyo Yanga kama Serikali inavyofanya ili ifanye vizuri kwenye michezo miwili ya fainali iliyobaki.
Baada ya kauli ya Rais Samia uongozi wa Yanga ulitoa taarifa ya kumshukuru: “Uongozi wa Yanga unapenda kutoa shukrani kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia ndege ya kusafiria kwenye mchezo wetu wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa nchini Algeria dhidi ya USM Alger.”
Wakati huo huo, Rais wa heshima na mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter ameipongeza Yanga kwa kuingia fainali na kuieleza kuwa Tanzania inajivunia kwa mafanikio hayo.
Mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali itachezwa Mei 28, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na mechi ya marudiano itachezwa Juni 3, mwaka huu nchini Algeria.
Yanga imekuwa timu ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati katika miaka ya karibuni kucheza fainali za michuano ya Afrika baada ya Gor Mahia ya Kenya kutwaa lililokuwa taji la Washindi Afrika mwaka 1987 na kucheza fainali mwaka 1979.
Simba waliwahi kucheza fainali ya michuano ya klabu Afrika mwaka 1993 wakati wa mashindano ya Kombe la Caf na kufungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast.