Milan, Italia
Baada ya kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, kocha wa Inter Milan, Simone Inzaghi sasa anamhofia mpinzani atakayekutana naye kwenye fainali kati ya Man City au Real Madrid.
Inter jana Jumanne ilifuzu hatua ya fainali baada ya kuwalaza mahasimu wake AC Milan kwa bao 1-0 jana Jumanne na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 baada ya ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.
Timu hiyo sasa inasubiri kucheza fainali na mshindi wa mechi ya leo usiku kati ya Real Madrid au Man City itakayopigwa kwenye dimba la Ittihad baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu.
Baada ya ushindi dhidi ya Inter Inzaghi (pichani juu) aliulizwa atapenda kukutana na timu ipi kati ya Man City na Real Madrid katika mechi ya fainali itakayopigwa Juni 10 mwaka huu kwenye dimba la Ataturk Olympic mjini Istanbul, Uturuki.
Kocha huyo hata hivyo hakutaka kuitaja kwa jina ni timu ipi ambayo itakuwa rahisi kwake badala yake alisema kwamba unapocheza na moja ya timu hizo wewe unaanza ukiwa timu ndogo.
“Ni jambo la kawaida unapoumana na City au Real kwanza unakuwa timu ndogo, lakini soka ni mchezo wa wazi, tulikutana na Real Madrid mwaka jana tukapoteza mechi mbili lakini tulicheza vizuri, Manchester City huhitaji kuwazungumzia, tutaona itakavyokuwa, yeyote atakayekuja ndio amekuja,” alisema Inzaghi.
“Yeyote tutakayekutana naye kwetu halitokuwa jambo zuri kwa sababu hizi ni timu mbili kubwa na zenye viwango vya kipekee, tutawaangalia hapo kesho (leo Jumatano), nitawaangalia kama vile naangalia mechi ya kwanza, ni dhahiri kwamba tutaifuatilia mechi yao kwa karibu,” aliongeza Inzaghi.
Man City inatarajia kutangazwa bingwa wa Ligi Kuu England (EPL) wikiendi hii iwapo Arsenal itapoteza mechi yake ya Jumamosi au City itashinda mechi yake ya Jumapili. Kwa upande wa Real Madrid imeshapoteza taji la La Liga ambalo limechukuliwa na mahasimu wao Barca.