Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki ameshinda bao bora la wiki la hatua ya nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Aziz Ki alifunga bao hilo kwenye ushindi wa mabao 2-0 walioupata Yanga dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Jumatano iliyopita. Bao jingine la Yanga lilifungwa na Bernard Morrison.
Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii leo Jumatano waliweka video ya bao alilofunga mchezaji huyo na kutangaza kuwa ndio bao bora la wiki la mkondo wa kwanza hatua ya nusu fainali.
“Aziz Ki anajua jinsi ya kuzifungua nyavu za wapinzani. Goli la wiki la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya nusu fainali limekwenda kwa mshambuliaji wa Yanga,” yaliambatanishwa maneno hayo kwenye video ya bao hilo.
Yanga leo Jumatano imeshuka kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg kwenye mchezo wa pili wa hatua hiyo dhidi ya Marumo na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Mabao ya Yanga katika mechi hiyo ambayo Aziz Ki alicheza akitokea benchi, yalifungwa na Fiston Mayele na Kennedy Musonda wakati bao pekee la Marumo lilifungwa na Ranga Chivaviro
Kimataifa Aziz Ki ashinda bao bora Caf
Aziz Ki ashinda bao bora Caf
Read also